Saturday, November 12, 2011

KWANINI MKULIMA MWAMWINDI ALIMPIGA RISASI DR.KLERUU:

Ndugu zangu,

Nimeamua kuiendeleza na kuimaliza simulizi ya Mwamwindi wa Iringa. Hii ni kutokana na ujio wa Gazeti la Kwanza Jamii mkoani Iringa na hamu ya wasomaji wengi kutaka kuifahamu historia ya mkoa wao.

Iringa ina historia ndefu ya harakati za mapambano ya kudai uhuru. Harakati za kijamii, kisiasa na kiuchumi. Wakati huu nchi yetu ikielekea kwenye kuadhimisha miaka 50 ya uhuru si vibaya tukakumbushana tulikotoka ili tuweze kuelewa tulipo sasa na tunakokwenda.

Hakika, simulizi ya Mkulima Said Mwamwindi aliyepambana na dola ni moja ya simulizi zilizowagusa wasomaji wangu wengi .

Ni simulizi iliyonifanya nihamasike kutafuta habari zaidi za WaTanzania mfano wa Mwamwindi ambao, hata kama huko nyuma jamii ilitakiwa iwaone kama wasaliti, lakini, jamii si mkusanyiko wa watu wajinga. Kuna walioulewa ukweli, waliamua kukaa kimya. Na wakati mwingine walisema na hata kuimba kile ambacho watawala waliwataka waimbe na kusema. Hata hivyo, mioyoyoni mwao, waliujua ukweli. Kuna walioimba huku wakilia mioyoni. Kuna waliosema huku wakisononeka mioyoni.

Huu ni wakati wa kujaribu kuusema ukweli ili tuweze kwenda mbele kama taifa. Simulizi ya Mkulima Said Mwamwindi ni jaribio la kuutafuta ukweli huo. Na hii ni simulizi shirikishi yenye kukukaribisha ewe msomaji, uje na unachokijua juu ya kilichotokea zaidi ya miaka 40 iliyopita. Mwamwindi ni kielelezo cha hali iliyokuwepo wakati huo. Mathalan, utekelezaji wa Sera za Ujamaa na kilimo cha ushirika ulitakiwa utekelezwe kwa kuzingatia mazingira ya kila mahala.

Inakuwaje basi kwa mkuu wa nchi unapomweka mkuu wa mkoa kijana anayeanza kwa kuwahutubia wakulima wakubwa mfano wa Said Mwamwindi habari za kilimo cha heka nne nne? Wakulima ambao tayari, hata kabla ya Uhuru wameweza kuwa na matreka na hata kuanzisha ushirika wao wa wakulima. Ndio, inazekena vipi kwa Mkulima wa shamba la ekari mia nne akajisikia furaha kuwa kwenye mkutano na mkuu wa mkoa anayezungumzia kilimo cha ekari nne nne? Mbinu gani ya kiuongozi ilihitajika ili kumfanya mkulima mkubwa kama Mwamwindi ashiriki na kuwasaidia wakulima wadogo wadogo?

Na hapa inaanza simulizi ya Mwamwindi;

Mwanzoni mwa miaka ya 1970 Mkulima said Mwamwindi alikabiliwa na shitaka la kumwua Dr Wilbert Kleruu, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa wakati huo.

Mshitakiwa Mwamwindi alijitetea kuwa alipokuwa anamwua marehemu Kleruu alirukwa na akili . Hivyo, akapotewa na fahamu ya kuweza kuelewa kile alichokuwa anakitenda. Jaji Onyiuke kutoka Nigeria aliukataa utetezi wa Mwamwindi kwa kutilia maanani kwamba baada ya mshitakiwa kughadhibishwa ndipo alipokwenda ndani kuchukua bunduki ambayo aliitumia kumwua marehemu.

Mwezi Oktoba mwaka 2010, nikiwa njiani kwenda Dodoma na Arusha, nilipita kijijini Isimani. Hapo ndipo yalipokuwa makazi ya Mwamwindi. Ni umbali wa kilomita zipatazo 40 kutoka Iringa Mjini. Kijijini Isimani Saidi Mwamwindi bado anaonekana ni shujaa kwa kukataa kunyanyaswa na Mkuu wa Mkoa. Inasimuliwa, kuwa ilikuwa siku ya Jumapili , tena siku ya Krismasi, pale Mkuu wa Mkoa, Dr Kleruu, alipofika Isimani na kumkemea Mwamwindi mbele ya wake zake kwa vile alifanya kazi za shamba siku ya Sikukuu.

Inasimuliwa, kuwa Dr. Wilbert Kleruu alifikia hata hatua ya kuanza kudhihaki makaburi ya mababu zake Mwamwindi akimwambia Mwamwindi: “Humu ndimo mlimozika mirija yenu”. Alifanya hivyo huku akionyesha makaburi yake kwa kutumia fimbo aliyoshika mkononi. Mwamwindi alikasirika sana. Akaficha hasira yake. Kutoka makaburini, Mwamwindi aliongozana na Kleruu hadi nje ya nyumba yake. Akamwomba Mkuu huyo wa Mkoa abaki nje. Mwamwindi akaingia ndani chumbani.

Mke wake Mwamwindi alimwona mume wake akichukua bunduki na kusimama dirishani. Mama huyo alidhani mumewe amepanga kwenda kuwinda. Kumbe, Mwamwindi alitokea dirishani na kumwelekea Kleruu aliyedhani Mwamwindi angetoka nje kwa kupitia mlangoni.
Basi, Mwamwindi akamlenga Mkuu wa Mkoa sawa kichwani. Dr kleruu alinyosha mikono juu na kuomba asemehewe. Mwamwindi alikaa kimya. Kisha akafyatua risasi. Kishindo kilisikika kijijini. Baada ya hapo, kwa mikono yake, Mwamwindi akaubeba mwili wa Mkuu wa Mkoa na kuuweka nyuma ya boneti ya gari alilojia mkuu huyo wa mkoa.

Mwamwindi alichukua kofia ya pama aliyovaa Kleruu. Akaivaa kichwani na kuanza kuendesha gari hilo hadi kituo cha polisi Iringa. Waliokutana na Mwamwindi njiani walimshangaa akiendesha gari hilo la Mkuu wa Mkoa akiwa amevalia kofia ya mkuu huyo. Hatimaye Mwamwindi akafika kituo cha Polisi.

Akatoka na kwenda mapokezi. Hapo akaripoti tukio kwa kutamka; " Nendeni mkamchukue mbwa wenu nyuma ya gari!".

Tukio lile bado linatuachia maswali? Je, ni kwanini Dr Kleruu alikwenda nyumbani kwa Mwamwindi siku ya Jumapili na hususan siku ya Krismasi?

Je, yawezekana Mwamwindi na Dr Kleruu walikuwa na ugomvi mwingine kabla ya tukio?

Kuna waliokuwepo na wanasimulia kana kwamba ilikuwa ni jana tu. Mmoja wa watu hao ni mwana wa Mkulima Said Mwamwindi aitwaye Amani Mwamwindi ambaye ndiye Meya wa Manispaa ya Iringa kwa sasa. Amani Mwamwindi anakumbuka nini juu ya siku hiyo? Fuatilia Simulizi hii Juma lijalo.

Maggid Mjengwa,
Iringa.

No comments:

Post a Comment