Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu mgogoro wa serikali na Madaktari, Ofisini kwake jijini Dar es salaam Machi 6, 2012.Picha na Ofisiya Waziri Mkuu.
Pia amewasihi madaktari hao kutoendelea na mgomo leo na badala yake waiachie Serikali iendelee kushughulikia madai yao, likiwamo suala la kubadili uongozi wa wizara hiyo na iwapo wataendelea na mgomo, watambue kuwa maisha ya Watanzania yako mikononi mwao.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Pinda alieleza kushangazwa na kitendo cha madaktari hao kung’ang’ania hoja ya kufukuzwa kwa Dk Mponda na Dk Nkya, wakati waliwasilisha mbele ya Serikali madai mengi na yanayoendelea kushughulikiwa na kutoa mapendekezo ya nini kifanyike.
Alisema alipokutana na madaktari hao aliunda Kamati iliyojumuisha sekta mbalimbali wakiwamo wajumbe wawili wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), wauguzi na wafamasia, kwa ajili ya kushughulikia madai ya madaktari hao na kamati hiyo ilishakamilisha kazi yake.
Hata hivyo, alisema katika mkutano wao wa mwisho na Serikali ulioongozwa kwa upande wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma, George Yambesi, madaktari hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa MAT, Dk Namala Mkopi, waligoma kuendelea na mazungumzo wakitaka viongozi hao wasimamishwe.
“Niliambiwa kuwa wakati kikao hicho kinaanza, madaktari waliweka masharti ya kutaka viongozi hawa wasimamishwe ndipo majadiliano mengine yaendelee, nikajiuliza kwa nini wang’ang’anie masharti haya wakati tayari Serikali ilishasema yanashughulikiwa?” Alihoji. Alisema anachofahamu ni kwamba viongozi hao wawili nafasi zao ni za kisiasa na mwenye mamlaka ya kuwateua ni Rais.
“Hivyo kitendo cha Mkuu wa Nchi kupewa saa 72 awe amewasimamisha kazi, kwanza mimi sikubaliani nacho na ninajua hata Rais mwenyewe hatakubaliana nacho,” alisema.
Alisema inafahamika wazi kuwa madai waliyotoa madaktari hao kwake yanafanyiwa kazi na mengi kama vile nyongeza ya posho, posho za mazingira hatarishi, mishahara, posho za usafiri na bima, yanazungumzika na kwamba utaratibu wa kuyafanyia kazi ulikuwa unaendelea.
Alitoa mfano kuwa madaktari hao walitaka posho ya sasa kwa kima cha juu kwa madaktari ya Sh 25,000 kwa siku iongezwe na kufikia Sh 50,000 huku wengine wakitaka ifikie Sh 80,000, jambo ambalo linaweza kushughulikiwa ingawa kwa kupitia kwanza bajeti na hali ya uchumi wa nchi.
“Ndiyo maana nashangaa wenzetu hawa kulileta suala hili leo, wakati tulishatoka nao mbali hadi kufikia kusimamisha kwanza Katibu Mkuu (Blandina Nyoni) na Mganga Mkuu (Deo Mtasiwa), ili kupisha uchunguzi huku madai mengine yakishughulikiwa, kwa masharti haya mapya labda kama wenzetu wana jambo lingine,” alisema.
Aliwaomba madaktari hao waiachie Serikali kazi ya kushughulikia madai yao na kuendelea na kazi leo, lakini wakiendelea na mgomo huo kwa kisingizio cha kuwasimamisha Dk Mponda na Dk Nkya haitaleta picha nzuri kwa Watanzania, kwa kuwa wao ndio waathirika wakuu.
“Kwanza jamani huyu Dk Mponda ndiyo kwanza ana mwaka mmoja na miezi kadhaa tangu awe Waziri wa Afya na mengi ya madai ya madaktari hawa yanaonekana wazi ni matatizo ya muda mrefu, hali ambayo kweli Serikali imeona na kuamua kuijenga sekta hiyo ya afya ili iwe na meno,” alisema.
Alisema amesikia na kupokea ujumbe mwingi kuwa madaktari hao wamepanga kugoma leo huku wakidai kuwa wataikomesha Serikali.
“Naomba watambue kuwa wanachofanya si kuikomesha Serikali, bali kuwakomesha wagonjwa, kwani wao ndio waathirika wakuu, naomba watumie busara na hekima na kurejea kazini, ili kuwalinda Watanzania wasio na hatia.” Alisema ni jambo linalosikitisha kuona madaktari hao ambao wanatambua umuhimu wao kwa Taifa hasa suala la afya, kutumia fursa hiyo ya maisha ya Watanzania kuibana Serikali, kwa kuwa wanafahamu wanaweza kufanya lolote wanalotaka.
Alisema kimsingi, zipo sheria za nchi ambazo zinaweka bayana masharti kwa sekta zinazogusa watu, ikiwamo ya afya wafanyakazi wake kutogoma, kwa kuwa waathirika zaidi wa migomo hiyo ni wananchi ambao hawana hatia. Aliwataka madaktari kutambua kuwa sheria katika eneo hilo iko makini na kuwasihi iwapo wanataka kugoma basi wagome kwa misingi ya kisheria.
“Ila jamani ninawaomba sana madaktari wasigome na kuacha watu wakifa kwa kisingizio cha watu wawili, watambue kuwa huwezi kumpa Rais masharti, hili halikubaliki si hapa tu hata nchi zingine.” Kuhusu Serikali imejipangaje iwapo madaktari hao watagoma leo, Pinda alisema haijajiandaa na lolote kwa kuwa inaamini wataalamu hao watatumia hekima na kuiachia Serikali ishughulikie madai yao na wao kuendelea na kazi.
“Lakini jamani tujipange kwa lipi, kwa kuwa Mponda hajaondoka? Basi kama ni hivyo kuna tatizo kubwa kuliko inavyodhaniwa.” Aidha Pinda alisema mpaka sasa hajafahamu athari za mgomo wa madaktari uliopita na kutaka swali hilo, waulizwe wahusika wenyewe wa sekta ya afya, kwa kuwa wao ndio wanaofahamu jinsi Watanzania walivyoumia.
Chanzo cha habari hii ni: http://www.habarileo.co.tz/
No comments:
Post a Comment