Ndugu zangu,
Nimeangalia TBC1 usiku huu. Nilikuwa na kiu ya kufuatilia kilichoendelea bungeni leo kwenye suala la Katiba. Maana, kuna wengi miongoni mwetu, kutokana na majukumu mengine, tunashindwa kufuatilia ' live' kinachoendelea bungeni.
Na hakika, TBC1 bado ni chombo cha habari cha umma kinachoheshimika. Naandika kuwaatadharisha TBC1, kuwa heshima yao inaweza kushuka kama hawataonyesha umakini kwenye mambo ya msingi ya kitaifa. Ona leo, kuhusu mjadala wa Muswaada wa Katiba, wabunge waliounga mkono hoja walipata coverage kubwa, mfano, tuliwasikia kwa sauti zao Ole Sendeka wa CCM na Hamad Rashid wa CUF.
Ilipofika zamu ya Mbunge Machali wa NCCR Mageuzi, basi, mtangazaji wa TBC1 ndiye aliyetwambia kwa ufupi sana alichosema mbunge huyo. Umma haukupewa nafasi ya kumsikia Mbunge Machali kwa sauti yake mwenyewe!
Tuwe wakweli kwa nchi yetu, kuwa ni mambo kama hayo ndiyo yenye kuchangia kupungua kwa imani ya umma kwa mchakato mzima wa kuratibu Katiba. Hapa kuna mawili, ama TBC1 wanashindwa kufanya kazi yao vema ya kuhabarisha umma au wanafanya kazi kwa maelekezo rasmi.
Ona, iweje habari ya ‘ abrakadabra’ ya misukule ya Iringa ipate nafasi kubwa kuliko sauti ya Mbunge wa NCCR Mageuzi anayetoa maoni yake kuhusu Muswaada wa marekebisho ya Katiba? Jambo muhimu kabisa kwa nchi yetu kwa wakati huu. Tujisahihishe ili tusonge mbele kama taifa moja.
Maggid,
Iringa,
Jumanne, Nov,15, 2011.
No comments:
Post a Comment