Thursday, August 25, 2011
AIRTEL YATOA TSH.MIL 15 KAMA SEHEMU YA UDHAMINI WAKE KATIKA ROCK CITY MARATHON 2011:
KAMPUNI ya Airtel Tanzania imetoa sh. mil 15/- kama udhamini wake katika mashindano ya riadha ya kilomita 21 yanayojulikana kama ‘Rock City Marathon 2011’ yatakayofanyika Septemba 4 mwaka huu Jijini Mwanza.
Akizungumzia udhamini huo Meneaja Uhusiano wa Kampuni hiyo Jackson Mbando alisema ni hatua inayothibitisha jinsi kampuni hiyo ilivyodhamiria kidhati kuinua michezo mbalimbali nchini.
Alisema pamoja na mambo mengine Airtel imekuwa na mikakati na programu mbalimbali zinazochangia kukua kwa sektta ya kichezo nchini na kwamba riadha ni sehemu ya michezo wanayoona inastahili kuwekewa nguvu na wadau.
“Wote mnajua tumekuwa na mchango mkubwa nchini katika kuinua michezo mbalimbali na udhamini wetu katika hili unadhihirisha dhamira ya dhati tuliyonayo katika hili na tutaendelea kufanya hivi kwa kadri uwezo utakavyokuwa unaruhusu”, alisema Mbando.
Wadhamini wengine ambao tayari wamejitosa katika mshindano ya mwaka huu ni pamoja na Geita Gold Mine, Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), New Africa Hotel, Mfuko wa Pensheni wa Taifa (PPF), Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bank M, MOIL, New Mwanza Hotel, Shirika la Hifadhi ya Wanyapori Tanzania (TANAPA) na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).
Mratibu mashindano hayo kutoka Kampuni ya Capital Plus International (CPI) Zaituni Ituja alisema wanaandaa mshindano hayo kwa mara ya tatu mwaka huu na kwamba mbio hizo zitaanzia uwanja wa CCM Kirumba kuelekea njia tofauti za Jiji la Mwanza na kumalizia katika uwanja huo.
Kuhusu zawadi alisema alisema washindi wa kilometa 21 watapata sh.500,000/-kwa pande zote mbili za wanaume na wanawake huku yule atakayevunja rekodi ya mwaka huu ya dakika 59 atapata zawadi ya jumla ya sh. Milioni Moja na wale watakaoshika nafasi ya pili watapata sh. 300,000/-
Watakaoshika nafasi ya tatu watapata sh. 200,000/- huku nafasi ya nne hadi 12 kila mmoja atapata sh.90,000/- na wale watakaoangukia katika nafasi ya 13 hadi 50 kila mmoja atapatiwa kifuta jasho cha sh. 30,000/- wakati washindi 21 wa mbio za Kilometa 5, Kilometa 3 kwa Walemavu, Kilometa 3 za Wazee na Kilometa 2 kwa Watoto watapatiwa sh. 25,000/- kila mmoja kama kifuta jasho.
“Kiujumla tumekuwa na maboresho makubwa katika zawadi kwa kuongeza wigo wa watu wanaozawadiwa na hii tumeifanya makusudi tukiwa na lengo la kuongeza hamasa kwa wote watakaoshiriki ili tuendelee kuamsha ari ya ushiriki na kuibua vipaji vya riadha nchini”, alisema.
Aliongeza kuwa tayari mikoa 14 imeonyesha nia ya kushiriki na ni faraja kwao na hiyo inathibitisha kukua kwa mashindano yenyewe mwaka hadi mwaka lakini pia inaonyesha ushindani utakuwa mkubwa zaidi.
“Tumeamua kuendelea kupanua wigo wa ushiriki mwaka huu kutokana na kutambua umuhimu wa michezo kwa rika mbalimbali lakini muhimu zaidi ni mapendekezo tofauti tuliyopokea kupitia wadau mbalimbali baada ya kumalizika kwa mashindano ya mwaka jana”, alisema Ituja.
Fedha zitakazopatikana kutokana na fomu za usajili zitaenda katika mfuko wa kuwasaidia watu wenye ulemavu mkoani Mwanza. Fomu kwa ajili ya kujisajili zitapatikana Ofisi za uwanja wa CCM Kirumba, Ofisi za CPI- DSM, Makao Makuu ya Chama cha RiadhaTanzania (RT) Dar es Salaam, Ofisi za MRAA Mwanza. Fomu za usajili pia zinapatikana katika tovuti ya www.rockcitymarathon.blogspot.com or info@capitalplus.co.tz.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment