Friday, January 27, 2012

TAMKO NA MSIMAMO WA CHADEMA KUHUSU MGOMO WA MADAKTARI NCHINI:

Mbunge wa Ubungo(Chadema)Mh John Mnyika.

Mgomo wa madaktari unaoendelea hivi sasa umedhihirisha kwamba tuna serikali dhaifu yenye ombwe la uongozi. Haiwezekani wananchi wakawa wanakufa kwa kukosa matibabu stahiki na wengine wakipata madhara kutokana na kuchelewa kupata matibabu sababu ya mgomo wa madaktari halafu viongozi wenye dhamana hawachukui hatua sahihi.

Rais Jakaya Kikwete ambaye ndiye mwenye dhamana kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 33 ndiye kiongozi wa shughuli za serikali na ibara ya 35 shughuli zote za utendaji wa serikali zinatekelezwa na watumishi wa serikali kwa niaba ya Rais; ameondoka kwenda nje ya nchi mgomo ulipoanza na hakuna kauli yoyote mpaka sasa toka kwa Makamu wa Rais wala kwa Ikulu.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda badala ya kwenda kwenye eneo la mgomo na kuzungumza na madaktari naye ameishia kuzungumza na vyombo vya habari. Waziri wa Afya Dk. Haji Mponda na Naibu Waziri Dk. Lucy Nkya nao jana wamezungumza na waandishi wa habari badala ya kwenda kukutana na madaktari na kuzungumza nao kuhusu madai yao ya msingi.

Kwa upande wetu CHADEMA tulitoa kauli tarehe 25 Januari 2012 ya kutaka serikali ichukue hatua na tuliona tuipe serikali nafasi ifanye kazi yake hata hivyo serikali haionyeshi kuupa uzito unaostahili mgogoro huu wenye kuathiri hali za wagonjwa na maisha ya wananchi katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Tuliacha kwenda katika eneo la mgomo kukutana na madaktari katika siku za awali kuepusha suala hili kutafsiriwa kuwa ni la kisiasa. Hata hivyo, kuchelewa kwa serikali kukutana na madaktari kunahitaji hatua za pamoja. Dhamira yangu kama mwananchi, mbunge katika mkoa wa Dar es salaam na kiongozi wa chama cha siasa naumizwa na hali inayoendelea. Ni vigumu kuweza kuendelea na majukumu ya kibunge na ya kichama katika masuala mengine wakati serikali iko legelege katika suala ambalo linahusu uhai wa wananchi wenzangu uko mashakani.

Hivyo nawajibika siku ya leo kuelekeza nguvu katika kuungana mkono na madaktari katika madai yao ili kuishinikiza serikali kuweza kutuma ujumbe mkubwa kukutana na madaktari leo au kesho. Na iwapo serikali haitakutana nao katika muda huo, itabidi uongozi wa kambi ya upinzani bungeni ukiwa ni serikali kivuli na uongozi mkuu wa CHADEMA ukiwa ni chama mbadala kuweza kukutana nao.

Natambua kwamba uzembe na ufisadi katika serikali kwenye sekta ya afya unaligharimu taifa na maisha ya wananchi. Hivyo, CHADEMA inaitaka serikali kukamilisha kwa haraka majadiliano na madaktari na kutimiza madai yao ili kuepusha madhara zaidi kwa umma.

Nawapa pole wananchi ambao wameathirika na migomo inayoendelea na kuzingatia kwamba mgomo huo umesababishwa na udhaifu katika serikali.

Natoa mwito kwa umma wa watanzania kuwaunga mkono madaktari na watumishi wengine wa sekta ya afya katika hospitali na zahanati za umma kama sehemu ya kuboresha huduma katika maeneo husika.

Madai ya madaktari na watumishi wengine wa sekta ya afya nchini yasiposhughulikiwa kwa wakati na kwa ukamilifu watumishi husika wanaweza wasiwe kwenye mgomo wa wazi kama ilivyo kwa baadhi ya hospitali na zahanati nchini lakini wataendelea na migomo baridi kwa kutoa huduma mbovu au kuacha kazi kwenye maeneo ya umma na wengine kwenda kufanya kazi nje ya nchi wakati kukiwa na uhaba wa watumishi nchini.

Aidha, pamoja na migomo inayoendelea, naendelea kutoa rai kwa madaktari na watumishi wengine wa umma kuhakikisha maisha ya wagonjwa walio katika hali ya hatari yanaokolewa.

Nimezungumza na viongozi wetu wakuu kuhusu suala hili na natoa mwito kwa wadau wote kuunganisha nguvu katika kuisimamia serikali kushughulikia madai ya madaktari na wafanyakazi wengine wa sekta ya afya kwa haraka ili kuepusha madhara zaidi kwa umma.

Wananchi wenzangu wa Jimbo la Ubungo na umma kwa ujumla uzingatie kwamba tangu Mwalimu Nyerere aondoke madarakani mwaka 1985, Serikali ya CCM imeongeza wingi wa majengo mbalimbali kwenye sekta ya afya hata hivyo imeshindwa kusimamia utoaji bora wa huduma za afya katika zahanati, hospitali na vituo vya afya. Kutokana na mfumo mbaya wa usimamizi wa sekta ya afya, misingi imara ya kuimarisha sekta ya afya iliyowekwa baada ya uhuru imevunjwa na kubomolewa ikiwemo katika masuala yanayohusu kujali maslahi ya watumishi wa umma katika sekta hii muhimu.

Hali hii imefanya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuwa na nakisi ya watumishi asilimia 48% na takwimu zinaonesha kuwa 18% ya wafamasia, 15% ya madaktari, 13% ya madaktari wasaidizi waliacha vituo vyao vya kazi na kwenda kutafuta kazi kwenye mashirika ambayo yanalipa mishahara mikubwa na mizuri. Nakisi hii itaongezeka zaidi iwapo madai ya msingi ya madaktari na watumishi wengine hayatashughulikiwa na serikali itaendelea kuchelewa kushughulikia migogoro na migomo mingine inayoendelea.

Ni imani yangu kwamba serikali ikiwa na dhamira inaweza kuongeza mishahara kwa watumishi wa sekta ya afya ili kuweza kuwavutia wataalamu kubakia nchini badala ya kwenda kugoma au kwenda kutafuta kazi nje ya nchi kutokana na malipo mazuri huko. Hii ni pamoja kuwezesha malipo ya mazingira magumu kutolewa kwa watumishi wa afya wanaofanya kazi katika maeneo na kada maalum.

Kwa sababu hii, leo sitashiriki kikao cha Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kinachoendelea ili kupata wasaa wa kufuatilia kwa karibu suala hili na kuwasiliana na viongozi wenzangu kwa ajili ya hatua zaidi za pamoja.

Wenu katika utumishi wa umma,

John Mnyika (Mb)

27/01/2012
.

No comments:

Post a Comment