Friday, January 13, 2012

CHADEMA: URAIS UTAAMRIWA KWA MAHITAJI YA UMMA NA SIFA ZA KIONGOZI SI UTASHI WA WATU/MTU BINAFSI:

Katibu Mkuu wa Chadema Dk Wilbrod Slaa.
 
KUMEKUWEPO taarifa zinazosambazwa kwa umma kupitia njia mbalimbali za upashanaji habari, zikiwa na nia ya kuonesha kuwa kuna mbio za kuwania urais ndani ya chama na kuwa kuna baadhi ya watu wanapewa nafasi kubwa kugombea nafasi hiyo, kiasi kwamba sasa ndani ya CHADEMA “hapatoshi”
kwa ajili ya kuwania urais.


Chama kinapenda kutoa taarifa sahihi kwa wanachama, wapenzi, washabiki wake na Watanzania wote kwa ujumla, juu ya suala hili ambalo linaweza kuiweka CHADEMA katika mizania moja vyama vingine au kuwafananisha viongozi wa chama hiki na viongozi wa vyama vingine ambao wamekuwa wakilifanya suala la kugombea nafasi ya urais kuwa linaongozwa na kuamriwa kwa utashi binafsi wa mtu, ukiongozwa na uchu na tamaa ya nafasi ya vyeo.



Kwa sasa ndani ya CHADEMA kitu hicho cha ‘kupamba moto’ kwa ajili ya kuwania urais hakipo na wala hakiwezi kuwepo. Hasa kwa sasa ambapo chama kimejikita kuzidi kujijenga kwa kutimiza wajibu wake, kama serikali mbadala inayosubiri kupata ridhaa ya wananchi kuongoza nchi.




Kwa muda huu, kwa CHADEMA suala muhimu ni namna ya kutafuta mizizi au vyanzo vya matatizo mbalimbali yanayoikabili jamii pana ya Watanzania na kisha kutafuta majawabu au masuluhisho ya kudumu, kwa kushirikiana na Watanzania wote wenye nia njema na nchi yao, kwa ajili ya maendeleo

ya watu. Hii ndiyo ajenda muhimu, chama kinasimamia na hakiwezi  kutolewa kwenye mstari kwa watu kukimbilia urais.


Kwa CHADEMA, siku zote suala la urais linategemea na kufuata mahitaji mapana ya Watanzania, kamwe haliwezi kuamriwa kwa kufuata matakwa,utashi au uchu wa watu/mtu binafsi. Na katika kufikia hatma ya

mahitaji/ maslahi mapana ya wananchi, chama hiki siku zote huamua kwa kufuata na kuzingatia katiba, kanuni na taratibu zake, si vinginevyo.

Ni uwezo na umakini wa kuzingatia mahitaji ya chama na maslahi mapana ya umma katika kuamua masuala mazito kwa mstakabali wa taifa, huku kikifuata katiba yake, kanuni na taratibu, ndiyo umekipambanua CHADEMA kuendelea kuwa chama makini, kinachoaminiwa kwa dhati na Watanzania, na kiupekee kuwa kinastahili kupewa ridhaa ya kuongoza nchi hii.



Mahitaji ya chama na ya Watanzania ndiyo yaliyotumika kupata wagombea urais wa CHADEMA katika chaguzi kuu mbili, mwaka 2005 na 2010. kwa kuzingatia mtazamo huo, mara zote hizo mbili, wagombea waliombwa, wala hawakuongozwa na uchu au tamaa ya madaraka.



Hali itakuwa hivyo hivyo wakati ukiwadia wa kumpata mgombea urais wa mwaka 2015, kamwe utashi, uchu au maslahi binafsi ya mtu hayawezi kupata/kupewa nafasi ndani ya CHADEMA. Kwa CHADEMA, urais si cheo, ni dhamana ya utumishi kwa umma, suala ambalo linazingatia masuala muhimu, ambayo ni mahitaji ya wananchi (nchi) na kisha sifa za mtu husika kuwa kiongozi wa nafasi hiyo.



Kwa sasa CHADEMA na viongozi wake makini hawawezi kuanza mbio za kusaka urais, badala yake, muda wa sasa unatumika kujikita katika kushughulikia na kutafuta ufumbuzi wa vyanzo vya matatizo ya jamii

yanayozidi kuongezeka, huku serikali ikiishia kushughulika na dalili/ matokeo, hivyo kukosa majawabu ya kudumu na kuishia kutoa lawama kwa wakosoaji wake.


Hivyo kinachopewa umuhimu ni utumishi kwa umma, kwa ajili ya maendeleo ya watu na si mbio za kusaka vyeo. Ni vyema hii dhana ya mtu kufuatwa na kuombwa, mara anapoonekana kuwa anafaa kuongoza, kulingana na mahitaji ya watu na sifa za nafasi hiyo, kama ambavyo imekuwa ikifanyika ndani ya CHADEMA, ikaenziwa na kufanywa kuwa ni namna bora ya kupata viongozi.


Daima, CHADEMA na viongozi wake makini, kitaendelea kuweka mbele kwanza kabla ya kitu kingine chochote, mapambano dhidi ya vyanzo vya matatizo kama vile umaskini (ugumu wa maisha), rushwa na ufisadi mwingine lukuki unaozidi kutafuna na kuangamiza taifa na watu wake, hali inayowafanya Watanzania kuwa katika mtanziko na mkwamo mkubwa kimaendeleo, miaka 50 baada ya uhuru, huku wakiwa ndani ya taifa lenye baraka tele za utajiri wa rasilimali na kila aina ya nyenzo muhimu inayohitajika kwa maendeleo ya watu. Hii ndiyo ajenda ya muhimu kwa sasa.



Imetolewa, Januari 8, 2012, Dar es Salaam


Kurugenzi ya Habari na Uenezi, Makao Makuu ya CHADEMA Taifa

No comments:

Post a Comment