Monday, December 19, 2011

KAULI YA MH ZOTTO KABWE JUU YA KUFUKUZWA KWA MH.DAVUD KAFULILA NCCR-MAGEUZI:


Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe.

Leo(Jana) kwa masikitiko makubwa sana nimesoma kwenye vyombo vya habari kwamba ndugu David Kafulila kavuliwa uanachama wa chama chake. Kwa hatua hii David anakuwa amepoteza Ubunge wa jimbo la Kigoma Kusini licha ya kwamba alichaguliwa na wananchi bila kujali vyama (NCCR-M wanachama wake huko Kigoma Kusini hawafiki hata asilimia 10 ya wapiga kura wote). Haya ndio madhara ya Katiba ya sasa. Katakana na historia ya kisiasa baadhi ya watu wanajaribu kunihusisha na matatizo ya chama cha NCCR-M. Napenda kuweka wazi kwamba sihusiki kwa namna yeyote ile na migogoro ya chama kile. 
Ninaomba nisihusishwe na mambo yasiyonihusu. Ni dhahiri kwamba kuvuliwa uanachama kwa David ni jaribio kubwa kwa mfumo wetu wa demokrasia kama ilivyokuwa huko nyuma wakati kina Erasto Tumbo walipovuliwa uanachama wa chama chao cha UDP. Ninaamini NCCR-M watamaliza matatizo yao kwa mujibu wa katiba ya chama chao na ndugu David Kafulila atazikabili changamoto hizi kama kiongozi kijana wa kisiasa na kuona hii kama fursa badala ya kukata tamaa. Ifahamike wazi kabisa kwamba David ni mtu huru mwenye mawazo yake na maamuzi yake. Kwamba sisi ni marafiki wa karibu na kwamba tunatoka mkoa mmoja haina maana kwamba lolote afanyalo ama nimemtuma au ninahusika.
Ninaheshimu misimamo yake na siku zote huwa nipo upande wa anayeonewa, kudhulumiwa na mnyonge. Msimamo huu wa msingi usiwape watu nafasi ya kunihusisha na mambo ya chama dhaifu kisicho na dira kama NCCR-M.

Kafulila akumbuke kwamba hakufukuzwa CHADEMA, alijiondoa mwenyewe. Milango yetu ipo wazi kwa mujibu wa Katiba, Kanuni na taratibu za chama chetu.

Ndg. Kabwe Zuberi Zitto, Mb

18 Disemba 2011.

No comments:

Post a Comment