Katibu wa machimbo ya Taru Cavin Kamtwela, akilalamika kwa waandishi wa habari katika mkutano huo, jinsi wanavyotakiwa kumpisha mwekezaji.
Mmoja wa wachimbaji wadogo akilalamika juu ya vitendo wanavyofanyiwa na serikali kwa kushirikiana na Shanta Mining, ili waondoke eneo hilo.
Wachimbaji wa dhahabu wakionyesha mawe yenye dhahabu, ambayo yametokana na kulipuliwa na baruti chini ya ardhi.
Dhahabu ikiandaliwa
Wachimbaji wadogo wakikusanyika kwenye eneo la machimbo ya dhahabu, katika kijiji cha Taru, wilayani Singida.
Wachimbaji hawa hupata mlo wao kwa kina mama kama hawa, waliopo katika maeneo hayo ya mgodi nao wakijitafutia riziki yao.
Na Elisante John ,Novemba 10,2011.
WACHIMBAJI wadogo wa dhahabu katika vijiji vya Taru na Sambaru, wilayani Singida, wamepinga kuondolewa kwa nguvu kwenye eneo lao, ili kumpisha mwekezaji wa madini, kutoka nje ya nchi, kampuni ya Shanta Mining Ltd.
Walitoa msimamo huo juzi, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye machimbo hayo katika kijiji cha Taru, kujadili eneo lao wanalotaka kuporwa ili kuipisha kampuni hiyo,kufungua mgodi mkubwa wa dhahabu.
Walieleza kusikitishwa na hatua ya serikali kumkumbatia mwekezaji huyo, badala ya wachimbaji wadogo kumilikishwa wao eneo hilo, ili wapatiwe vibali halali, kwa ajili ya kuendesha kazi zao kisheria.
Wakizungumza katika mkutano huo, mwenyekiti wa kitongoji cha Taru Emmanuel Sawa,katibu wa wachimbaji hao Cavin Kamtwela na mchimbaji Said Hamad Sabodo,walidai kuvumbua eneo hilo, baada ya kutolewa kwa nguvu eneo linguine, ambalo pia walielezwa kumpisha Shanta.
Kutokana na mgogoro huo, wameomba msaada kutoka kwa mashirika, asasi za kiraia, watu na wanaharakati wanaojishughulisha na utetezi wa haki za binadamu, kwenda ili kujionea hali halisi na baadaye wasaidie katika mapambano hayo.
Kamishina msaidizi wa madini kanda ya kati ambayo ofisi zake zipo mkoani Singida, Manase Mbasha alisema kuwa, wachimbaji hao wakiondoka kwenye eneo hilo, watapatiwa lingine, baada ya kumpisha mwekezaji huyo.
Afisa madini huyo alifafanua kuwa, eneo linalotarajiwa kutumika kwa ajili ya kufungua mgodi, linajumuisha vijiji vya, Sambaru, Taru na Samumba, katika halmashauri ya wilaya ya Singida.
Kwa mujibu wa Mbasha, mwekezaji huyo ameomba leseni tatu kwa ajili ya kufungua mgodi, na tayari amemaliza shughuli za utafiti tangu oktoba mwaka huu, kazi aliyoianza mwaka 2003.
No comments:
Post a Comment