Wednesday, October 19, 2011

LOWASSA ACAHARUKA:







Peter Saramba na Moses Mashalla, Monduli
WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa amevunja ukimya na kuzungumzia tuhuma mbalimbali zinazoelekezwa kwake, huku akisisitiza kuwa sasa amechoka kukashifiwa.Alisema kuanzia sasa hatakubali kuchafuliwa jina lake na mtu yeyote au chombo chochote cha habari na atakayefanya hivyo, ajiandae kukabiliana na mkono wa sheria.

Lowassa alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake katika Kijiji cha Ngarash Wilaya ya Monduli, Arusha kuhusu tuhuma mbalimbali zinazoelekezwa kwake, ikiwamo ya kuandaa na kuongoza mpango mkakati wa kumhujumu Rais Jakaya Kikwete.

“Imetosha. Sasa nimeamua kukabiliana na yeyote atakayenichafulia jina na kunizulia mambo ya uongo. Nitatumia vyombo vya sheria na tayari nimewaelekeza mawakili wangu kufanya hivyo,” alisema,

“Baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu sasa, nimeamua kuanza kuchukua hatua mbalimbali za kisiasa na kisheria ambazo naamini zitatoa majibu sahihi dhidi ya wale wote walio nyuma ya ajenda hizi chafu kwa lengo la kuweka kumbukumbu sawia ndani ya chama changu na kwa jamii nzima ya Watanzania ambao kwa muda mrefu wamelishwa mambo mengi ya kizushi na wakati mwingine ya hatari dhidi yangu,” alisema.

Alisema tayari amepanga kuanza kuwasiliana na kuwasilisha malalamiko yake kwa mamlaka husika zinazosimamia mienendo ya kimaadili na weledi wa kitaaluma wa vyombo vya habari kama vile Msajili wa Magazeti na Baraza la Habari Tanzania (MCT).

“Kama hiyo haitoshi, baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu nimeshaanza kufikiria na kujipanga kuanza kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waandishi wa habari na wahariri ambao kwa makusudi wameamua kutumia vibaya uhuru wa habari ambao serikali imeutoa. Naamini sote tunakubaliana kuwa uhuru usio na nidhamu ni fujo.

Katika mkutano huo, Lowassa pia alikanusha madai kuwa hivi sasa yeye na baadhi ya wanaCCM, wanakusanya taarifa na vielelezo vya mabaya ya Rais Kikwete ili kuyawasilisha kwenye vikao vya chama.

Alisema katika mkakati huo, mahasimu hao wamekuwa wakivitumia baadhi ya vyombo vya habari na kufikia hatua ya kudai kuwa ameanza kuandaa orodha ya kile anachokiita madhambi ya Rais Kikwete ambayo wanadai kuwa amepanga kuyasoma wakati wa kikao kijacho cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM.

Alisisitiza kuwa ni jambo lisiloingia akilini kumhusisha yeye na kile kinachoitwa mkakati wa kumhujumu Rais Kikwete au CCM ambacho alisema ni mbunge anayetokana na chama hicho na kiongozi wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.

“Kuhusu hili, napenda kusema kwa uwazi kwamba, mbali ya ukweli kuwa sijapata kufikiria hata mara moja kuhusu hicho wanachokiita mabaya au madhambi ya Rais, sina na wala siijui hiyo wanayoitaja kuwa ni orodha ya mabaya ya namna yoyote dhidi ya Rais Kikwete,” alisema na kuongeza:

“Siyo kweli. Nampenda, namwamini na kumheshimu Kikwete ambaye urafiki wetu haukuanzia barabarani kama baadhi wanavyodhani. Kwanza sijui mabaya ya mheshimiwa Rais. Najua mazuri yake mengi lakini siyo mabaya, hivyo sina nia ya kuyatafuta. Siwezi kumhujumu Rais wala chama changu. Naamini hata mheshimiwa Kikwete pia hawezi kuamini uongo huo.”

Alisema awali, alikuwa akiyapuuza madai mengi yanayoelekezwa kwake lakini amelazimika kuvunja ukimya kwani uongo ukizungumzwa mara nyingi bila maelezo sahihi kutolewa, unaweza kugeuka kuwa ukweli na watu wakauamini.

Richmond na kujivua gamba

Kuhusu tuhuma za kampuni ya kufua umeme ya Richmond na falsafa ya kujivua gamba, Lowassa alisema atazizungumzia muda mwafaka ukifika lakini, akasisitiza kuwa atafanya hivyo kupitia vikao rasmi vya chama.

“Mimi nimetumikia CCM kwa takriban maisha yangu yote tangu nilipohitimu Chuo Kikuu Mlimani mwaka 1977. Ni kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja pekee ndicho nimekuwa nje ya mfumo wa chama nilipokuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC). Najua kuwa kupitia vikao ndiyo mtu unaweza kujenga hoja kukabiliana na zile usizozikubali,” alisema.

Alisema hataki kuzungumzia masuala hayo nje ya vikao kukwepa kufanana na baadhi ya viongozi wanaofanya hivyo kwa kutumwa na maslahi na utashi binafsi kwa lengo la kujipatia umaarufu na kuchafua wengine.

Maandamano ya UVCCM Arusha

Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli alikana kuhusika kwa namna yoyote na maandamano na malumbano yanayoendelea sasa ndani ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), unaomhusisha Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha, James Ole Millya na makundi mengine akisema kipindi yanatokea alikuwa Ujerumani kwa matibabu.

Hata hivyo, alishauri sauti za vijana zisipuuzwe kwani kufanya hivyo ni hatari kwa chama na taifa kwa ujumla kutokana na uwezo wa kundi hilo katika kufikiri, kuamua na kufanya mambo.

“Mzee Kingunge (Ngombale) alitufundisha kuwa vijana damu yao inachemka haraka na uamuzi na matendo yao yanafanyika kwa mtindo huohuo damu yao inavyochemka. Jambo muhimu ni kuwasikiliza, kujadiliana nao na kuwarekebisha kwa amani pale wanapokosea, kamwe wasipuuzwe wala kukaripiwa na kukandamiza mawazo yao,” alisema Lowassa.

Alitoa mfano wa maandamano waliyofanya enzi zao za ujana kupinga ziara ya mmoja wa mawaziri wa Marekani aliyetembelea nchini akisema licha ya kusukwasukwa na polisi, Mwalimu Julius Nyerere na Serikali yake haikupuuza hata kidogo hisia, mawazo na kitendo chao.

Alisema iwapo kuna uvunjifu wa sheria uliotokea katika harakati za vijana hao kuwasilisha mawazo na kutekeleza majukumu yao ni vyema sheria ikachukua mkondo wake bila kuonekana wanatiwa kashkashi, kwani hakuna aliye juu ya sheria.

Ugumu wa maisha na ukosefu wa ajira

Akirejea kauli yake aliyowahi kuitoa kuhusu ugumu wa maisha na ukosefu wa ajira kwa vijana nchini, Lowassa alisema tatizo hilo ni bomu linalosubiri muda wa kulipuka, iwapo hatua madhubuti na za haraka hazitachukuliwa.

“Kama taifa tufanye uamuzi mgumu wa kukopa fedha kutoka taasisi za ndani na nje, tujenge viwanda badala ya kusubiri uwekezaji kutoka nje ambako nako kuna tatizo sawa na hili linalotukabili. Waasisi wetu walifanya hivyo na kufanikiwa. Naamini sisi pia tunaweza tukiwa na nia thabiti ya kukuza uchumi wetu na kuongeza ajira kwa vijana wanaohitimu katika taaluma mbalimbali.”

Alisema hata Marekani na nchi za Ulaya zinazohimiza na kutekeleza sera ya uchumi wa kibepari, zimeanza kuchukua hatua zinazofanana na zinazotekelezwa katika ujamaa kwa kusaidia taasisi na kampuni za nchini mwao ili kukuza uchumi wao na kulinda ajira za wananchi.

Kampeni za urais 2015

Akionyesha kushangazwa na kitendo cha mjadala wa mrithi wa Rais Kikwete kutawala duru za siasa nchini sasa mwaka mmoja tu tangu kufanyika uchaguzi mkuu, Lowassa alisema hiyo: “Si salama kwa nchi wala amani yetu kila jambo nchini kutawaliwa na mjadala wa urais mwaka 2015.”

“Tumeacha kujadili mustakabali wa taifa kwa kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayoikabili jamii yetu na hili ni changamoto kubwa kwa vyombo vyetu vya habari ambavyo vinawajibu wa kuendeleza mijadala yenye tija kwa taifa, badala ya kukubali kutumika na wanasiasa wenye malengo yao binafsi.”

Alivitaka vyombo vya habari kuchukua jukumu la kuongoza mijadala ya kusaidia jamii kutafuta ufumbuzi wa ajira kwa vijana, uchumi na kulinda amani, utulivu na mshikamano alioeleza kuwa umeanza kutikiswa kwa vitendo na maneno ya watu wachache wenye malengo binafsi dhidi ya maslahi ya umma.

Habari na picha kutoka gazeto la MWANANCHI: 

No comments:

Post a Comment