Wednesday, August 10, 2011

NAIBU KATIBU MKUU WA UMOJA WA MATAIFA, DK.ASHA-ROSE MIGIRO,AZINDUA MPANGO WA KITAIFA WA KUSHUGHULIKIA UKATILI KWA WATOTO:

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bi. Asha Rose Migiro akizungumzia umuhimu wa Taifa kusimamia haki ya mtoto ya kuishi kwa amani na furaha bila kufanyiwa Ukatilii wa aina yoyote katika Kilele cha uzinduzi wa ripoti ya Utafiti na Mpango wa Kitaifa wa kushughulikia "Ukatili kwa Watoto" na mpango wa Udhibiti wa Taifa. 

Pichani Juu na Chini Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Taifa Dkt. Asha Rose Migiro na Waziri wa Maendeleo ya jamii, Jinsia na Watoto Mh. Sophia Simba wakizindua rasmi RIPOTI YA UTAFITI NA MPANGO WA KITAIFA WA KUSHUGHULIKIA "UKATILI KWA WATOTO" NA MPANGO WA UDHIBITI WA TAIFA.
Katikati ni Mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu Umoja Mataifa Bi. Asha Rose Migiro,  wa pili kushoto ni Waziri wa Maendeleo ya jamii, Jinsia na Watoto Mh. Sophia Simba, wa kwanza kushoto Waziri wa Elimu na mafunzo ya ufundi Dkt. Shukuru Kawambwa, wa Pili Kulia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI (Elimu) Bw. Majaliwa Majaaliwa na wa Kwanza Kulia ni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Haji Mponda kwa pamoja wakikaribishwa maandamano yaliyokuwa yakiingia katika viwanja vya Karimjee.
Mabalozi wawakilishi wa nchi mbalimbali nchini wakifuatilia uzinduzi wa ripoti hiyo.

 
Raia na watu mbalimbali kutoka taasisi za Kimataifa na  Kitaifa wakifuatilia kwa umakini kilele cha uzinduzi huo.
Watoto wa Shule mbalimbali za msingi wakiandamana katika sherehe za uzinduzi wa ripoti ya Utafiti na Mpango wa Kitaifa wa kushughulikia "Ukatili kwa Watoto" na mpango wa Udhibiti wa Taifa.


HOTUBA YA NAIBU KATIBU MKUU UMOJA WA MATAIFA
UZINDUZI WA RIPOTI YA UTAFITI NA MPANGO WA KITAIFA WA KUSHUGHULIKIA ‘UKATILI KWA WATOTO’ NA MPANGO WA UDHIBITI WA TAIFA

Tanzania, 9 Agosti 2011

[Salamu]
Wapendwa watoto wetu,
Mheshimiwa Sophia Simba,
Waheshimiwa Mawaziri wote mliofika hapa,
Wawakilishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na
Wawakilishi wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar,
Waheshimiwa Wabunge mlioko hapa,
Waheshimiwa Madiwani,
Viongozi wa taasisi za kiraia na zisizo za kiserikali,
Mabibi na mabwana,

Ninayo furaha kubwa sana kuwa hapa pamoja nanyi leo hii
katika tukio hili muhimu na la kihistoria kama alivyosema
Mheshimiwa Sophia Simba.

Lakini nina furaha ya pekee kuwa miongoni mwenu kwa sababu mimi ni Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ninayetokana na nchi hii nzuri.

Napenda awali kuchukua fursa hii kuishukuru taasisi ya
kuthibiti magonjwa ya Marekani - Centre for Disease Control
na pia kukishukuru Chuo Kikuu cha Muhimbili kwa kuendesha utafiti huu wa kipekee.

 Nawapongeza pia wataalamu wote walioshiriki uchunguzi huu unaofungua ukurasa mpya wa sayansi.

Aidha naipongeza Serikali ya jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa kuunga mkono juhudi zao na kutoa hadharani
matokeo ya uchunguzi huo.

 Kwa uzinduzi huu tunaandika historia kwani haijawahi kutokea katika Afrika nzima; kufanyika utafiti na uzinduzi unaoibua ushahidi kama huu unaoonyesha jinsi unyanyasaji wa watoto wa kike na wa kiume ulivyoenea katika jamii yetu.

Takwimu zilizopatikana zinaonesha unyanyasaji wa watoto
katika sura zake zote, iwe ni kupigwa, kutukanwa, kusimangwa au kunajisiwa.

Na tumeona hapa hata kubebeshwa mizigo mizito.

Takwimu hizi zinatia huzuni, lakini ni lazima tuzitazame na
tuzitizame kwa macho mawili na kuzitafakari ili tuweze
kubuni njia madhubuti za kukabiliana na unyanyasaji huo.

Ili tuweze hatimaye kukomesha kabisa unyama huu, ni lazima
tufahamu kiini na ukubwa wa tatizo lenyewe.

Ufahamu huo utapatikana kwa kuwa makini katika ukusanyaji wa takwimu, kufanya uchambuzi wa kina na kuzungumzia kwa uwazi yale tunayoyabaini kutokana na uchambuzi huo.

Aidha tutakapokuwa tumeng’amua kiini cha tatizo tutaweza
kutunga sera zitakazotuwezesha kubuni mikakati imara ya
kukomesha tatizo hilo ikiwa ni pamoja na kutenga fedha za
kutosha kwa ajili ya utekelezaji.

Kwa kuwa tunayo dhamira ya dhati ya kulinda maslahi ya
watoto wetu, yote hayo yanawezekana.

Umoja wa Mataifa unaona fahari kuwa unasimamia haki ya
mtoto ya kuishi kwa amani na furaha bila kufanyiwa ukatili
wa aina yeyote ile.

Tanzania ni moja ya nchi zilizomo katika kampeni ya Umoja wa Mataifa ya kukomesha ukatili kwa watoto.

Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Mtoto
ulipitishwa mwaka 1990, na Tanzania ilijiunga mara moja
katika mwaka huo huo mkataba ulivyopitishwa. Naipongeza
Tanzania kwa hatua hii muhimu na natumaini Mheshimiwa
Sophia Simba utafikisha ujumbe huu muhimu kwa viongozi
wa taifa letu.

Kwa upande wetu, Umoja wa Mataifa umejitahidi sana
kushughulikia suala hili kwa kusaidiana na watu mbali mbali
miongoni mwa wataalamu na watetezi wa haki za watoto
pamoja na mashirika mengine ya Umoja huu.

Tumejitahidi kwa nguvu zetu zote kukabiliana na jukumu hilo zito la kukomesha ukatili kwa watoto.

Ndio maana, nimepata ari kubwa kuona kuwa Tanzania nchi
yangu mwenyewe inachukua hatua madhubuti kukomesha
ukatili kwa watoto.

 Tukumbuke kuwa hapa Tanzania nusu yake ni watoto. Watoto ni hazina kubwa ya taifa hili kwani wao ndio kiungo kati ya kizazi na kizazi katika uhai wa taifa.

Kwa hiyo basi tukiwalea na kuwalinda watoto wetu kwa jicho
la huruma na mapenzi tutakuwa na uhakika wa kujenga taifa
lenye kusimamia haki na ustawi wa watu wake wote.


 Aidha wahenga walisema kuwa watoto wa leo ndio viongozi wa kesho, basi tutayarishe viongozi watakaokidhi utashi huo.
Ndugu zangu, mtoto anayeishi kwa wasiwasi, akihofia kuwa
wakati wowote anaweza kupigwa, kusimangwa au
kunajisiwa, hatakuwa na maendeleo mazuri shuleni kwa
sababu atakosa utulivu unaotakiwa katika kufuatilia masomo.

Aidha mtoto huyo atakuwa hana imani na mtu yeyote,
atakuwa anamshuku kila mtu kuwa anaweza kumdhuru.
Mtoto anayeishi kwa wasiwasi wa kutokuwa na uhakika wa
usalama wake, atakuwa kila wakati yuko katika hali ya kutaka
kujihami dhidi ya jamii ambayo anaiona haimtendei haki wala
haimlindi anapohitaji ulinzi.

 Aghalabu kujihami huku kunachukua sura ya utovu wa nidhamu au uasi kwa jamii.

Mabibi na mabwana, ripoti hii inatuonesha mambo ya
kustuwa kweli kweli. Kuna taarifa za kukithiri kwa ubakaji.

Tunaambiwa kuwa katika kila wasichana kumi, kuna
wasichana watatu waliobakwa kabla hata hawajafikia umri wa
miaka 18.

Wasichana hawa ndio tunawategemea kuwa wazazi
na viongozi wa taifa hapo baadaye, tutarajie nini basi
wanapotendewa uovu kama huu? Wanaweza wakapata athari
za kisaikolojia kiasi kwamba itakapofika wakati wao wa kuwa
wazazi, wakawa na woga wa kudumu kuhusu masuala ya
kujamiiana na afya ya uzazi.

 Isitoshe, katika hizo harakati za kubakwa msichana anaweza kuambukizwa Virusi ya Ukimwi - VVU au magonjwa mengine ya aina hiyo.

Ni dhahiri kwamba tunalo jukumu la kukomesha kwa nguvu
zetu zote ukatili wa kubaka na kunajisi vijana wetu wa kike na
wa kiume. Kwa mujibu wa utafiti mbali mbali, na kama
nilivyokwishasema vitendo hivyo ndio njia kuu ya kuenea
kwa VVU na UKIMWI wenyewe na magonjwa megine
yanayoambukizwa ka njia ya kujamiiana hapa Tanzania.

Ndani ya ripoti hii tunayoizindua leo, zimo pia taarifa za
kutisha kuhusu ukatili unaofanyika shuleni. Imeelezwa kuwa
zaidi ya nusu ya wavulana na wasichana wamefanyiwa
vitendo vya ukatili na waalimu wao.

Takwimu zinaonesha kuwa katika kila wasichana kumi, kuna msichana mmoja aliyenyanyaswa kijinsia na mwalimu wake. Hali hii haifai haifai, haifai kabisa; tusiivumilie hata kidogo.

Tanzania ina maendeleo mengi ya kujivunia hususan upande
wa kutoa elimu, hasa kwa wasichana. Na ninafurahi kwamba
katika uzinduzi wa taarifa hii muhimu tunayo timu nzima
hapa ya viongozi wa serikali akiwemo Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi Dokta Shukuru Kawambwa.

 Lakini haitoshi tu kuwapeleka watoto shule; lazima tuhakikishe kuwa huko shuleni kuna mazingira salama, yanayomwezesha mwanafunzi kuelekeza nguvu zake katika masomo na sio kuhangaikia usalama wake.

Uchunguzi huu umeonesha kuwa watoto waliofanyiwa ukatili
nao huwa wakatili wanapokuwa watu wazima. Kwa maana
hiyo tusipoweza kuzuia ukatili kwa watoto wa leo basi
tunaendeleza ukatili katika vizazi vijavyo.

Ukatili ni kama ugonjwa. Tukipuuza ukatili unaofanyiwa
watoto wetu, ukatili huo utaenea na kusambaa, na mwishowe
utazoeleka na kuonekana kama kitu cha kawaida katika jamii.
Aidha ukweli mwingine uliojitokeza katika utafiti huu ni kuwa
mara nyingi watoto wanafanyiwa ukatili na ndugu na jamaa
wa karibu ambao ndiyo walipaswa kuwa walinzi wao.

 Hii ni dosari kubwa katika jamii. Ni lazima ulinzi na usalama wa watoto uwe ni wajibu wa jamii nzima. Hatuna budi kujenga jamii ambayo haivumilii, na inachukia vitendo vya ukatili kwa watoto.

Ni lazima tujenge jamii inayojipa jukumu la kukemea,
kulaani na kuwaadhibu wale wote wanaotenda ukatili huo.

Ingawa ni muhimu kuwa na sera zinazolinda usalama na
maslahi ya watoto, jambo kubwa zaidi ni kuleta mabadiliko
katika fikra za watu. Watu waweze kuwa na mtazamo sahihi
kuhusu suala hilo.

Na hapa napenda nitumie mfano ambao hata Mheshimiwa Sophia Simba ameuzungumzia. Kwa mfano, watu waweze kuelewa kwamba kumchapa mtoto kunabomoa zaidi ari yake kuliko kujenga nidhamu yake.

Na nafurahi kwamba serikali inaangalia upya adhabu ya
viboko na kama nimewasikia vizuri waheshimiwa mawaziri
hapa, adhabu hiyo ipo mbioni kufutwa. Utafiti umeonesha
pia, watoto wanaotendewa vitendo vya ukatili na
udhalilishaji, mara nyingi hukaa kimya bila ya kutoa taarifa
katika vyombo vinavyoweza kuwalinda, kwa hiyo hawanufaiki
na huduma ambazo wanastahili kuzipata kutoka katika
vyombo hivyo.

Hivyo basi ni lazima turejeshe imani ya watoto wetu katika
vyombo hivyo. Tujenge mazingira ya kuwapa uhuru wa
kujieleza wakijua kuwa watasikilizwa kwa faragha, taarifa zao
zitaheshimiwa na watalindwa ipasavyo.
Vile vile ndugu zangu hatuna budi kuandaa mazingira yaliyo
salama, yanayowasaidia watoto – na muhimu zaidi –
yanayowapa watoto fursa ya kutoa taarifa za siri kuhusiana
na ukatili.

 Katika hili Polisi ni chombo kimojawapo muhimu.
Ninafurahi kwamba Inspekta Jenerali wa Polisi Saidi Mwema
ametuma mwakilishi wake kuwa hapa na naona timu
nyingine ya wanajeshi la Polisi wakiwa miongoni mwetu.
Ninafurahi kufahamu kwamba Jeshi la Polisi Tanzania lipo
mstari wa mbele katika mapambano haya. Nawapongeza
Polisi kwa uwajibikaji huu na kwa kuhakikisha kuwa watoto
wanapewa nafasi salama ya kueleza yaliyowasibu kwa ukweli
na uwazi, bila woga wala haya, wakiamini kuwa watasikilizwa
kwa dhati.

Hali kadhalika tuhakikishe kwamba mahakama zetu
zinawapunguzia watoto dhahama kwa kuweka utaratibu bora wa kusikiliza haraka mashauri yanayofikishwa kwao na
watoto wenye ujasiri wa kujitokeza kutoa taarifa. Kwa mara
nyingine napenda pia nitambue kuwapo kwa baadhi ya
viongozi wa mahakama, nimemuona hapa mheshimiwa Jaji
kwa hiyo tunatumaini kwamba ujumbe huu utakuwa umefika.
Wazazi, walezi na waalimu kwa upande wao wasisite kutoa
taarifa kwenye vyombo vinavyohusika mara tu wanaposhuku
kuwa mtoto fulani amefanyiwa ukatili au kunyanyaswa na
mtu yeyote yule; awe mzazi wake, mwalimu wake, jirani au
jamaa ili kuwanusuru na madhara zaidi.

Ninaipongeza tena Serikali ya Tanzania kwa kuanzisha
huduma motomoto ya simu. Nimetaarifiwa kuwa tayari kuna
namba imeshasajiliwa na kwamba itazinduliwa katika siku
zijazo. Watoto kama hamna taarifa, mimi nimeambia kuna
namba 116, namba ambayo imesajiliwa lakini bado haijaanza
kutumika na hiyo ni hatua muhimu. Hii ni huduma ya bure ya
Msimu inayopatikana kwa saa 24 kwa ajili ya kutoa taarifa za
unyanyasaji wa watoto. Tunaomba jeshi la polisi liharakishe
uzinduzi na matumizi ya huduma hii muhimu.

Huduma hii inatoa fursa kwa kila mwananchi kutoa taarifa
pale anapoona au anaposhuku kuwa kuna mtoto amefanyiwa
ukatili au kunyanyaswa . Basi hakuna sababu tena ya kukaa
kimya!

Tukiitumia huduma hii ya simu kikamilifu tutaweza kuwanusuru watoto wengi. Ili kufanikisha matumizi ya
huduma hii tunahitaji kuwa na fedha za kutosha na watendaji
wa kutosha waliopata mafunzo stahiki.

Tunahitaji pia kuimarisha huduma nyingine zenye manufaa
katika ulinzi na usalama wa watoto, kama vile huduma za
ushauri na huduma zinazokidhi mahitaji mahsusi ya watoto
na vijana.

Tayari Serikali imeshachukua hatua muhimu kwa
kutunga na kupitisha Sheria ya Mtoto ambayo pia nafurahi
kwamba Baraza la Watoto limeweza kufahamu kwamba
sheria hii imepitishwa. Sasa yatupasa kuongeza juhudi.
Nimefurahi kwamba Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na
Watoto – ambayo ni wizara ninayoienzi sana kwa kuwa
niliisimamia kwa miaka mitano – ndiyo iliyoshika hatamu
katika kutekeleza mpango-mkakati wa kitaifa.

Mpango huu wa miaka mitano wa Kuzuia na Kushughulikia Ukatili Kwa Watoto ni mwanzo madhubuti kabisa.

Tunapoungana na washirika wetu – washirika kama ninyi
mlio hapa – tunaweza kwa pamoja kukomesha tatizo hili kwa
watoto. Kila mshirika ana dhima yake. Vyombo vya habari
vinaweza kuufahamisha umma. Asasi za kidini zinaweza
kuwajenga watu kimaadili. Asasi za Kiraia zinaweza
kuhamasisha jamii kuchukua hatua zinazostahiki. Sisi sote
tunaweza kutumia ushahidi ulio katika utafiti huu ili kujenga
mazingira salama kwa ajili ya watoto, na kusiwepo kamwe
aina yoyote ya ukatili na utesaji.

Mabibi na mabwana,
Mimi nikiwa Mtumishi wa Umoja wa Mataifa, na mwanasheria,
na muhimu zaidi nikiwa mzazi, natambua kwamba si rahisi
kuleta mabadiliko mpaka kwanza tukubali kwamba lipo tatizo.
Kukiri kuwa kuna tatizo ni jambo gumu lakini Tanzania tayari
imechukua hatua hiyo ngumu kwa kuanzisha utafiti huu na
na kusambaza matokeo yake.

Ninajivunia nchi yangu Tanzania kwa kuonesha uongozi wa
kweli – kutambua kuwepo kwa tatizo na kusimama kidete kukabiliana na tatizo hilo sugu, na kuweka nia ya
kulitokomeza kabisa.

Mwezi Juni tu mwaka huu, katika wilaya ya Hai, binti wa
miaka 15 alipewa ulinzi. Kwa miaka mitatu tangu mama yake
afariki, binti huyu maskini alikuwa akinajisiwa kwa nguvu na
baba yake wa kambo.

Lakini aliweza kupata ulinzi shuleni kwa sababu alijitokeza mwalimu mwenye msimamo sahihi. Mwalimu huyo
alimpeleka kituo cha polisi.


 Shauri lake likashughulikiwa haraka. Na hatimaye binti aliweza kusema maneno yafuatayo,

ninanukuu; “Nilijisikia salama mahakamani kwa kujua
kwamba baba yangu wa kambo hatanifanyia ukatili huo
tena.” Baba huyu alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.
Binti huyo sasa yuko huru, anaendelea kuishi na mama yake
mlezi anayemjali na kumpenda. Kisa hiki kinatuonesha nini?
Pale amabapo vyombo husika vimesimama imara, Polisi,
mahakama, shule kama ukatili huu umefanyika shule, wazazi
na wanajamii wakiungana pamoja, kwanza tutaweza
kuwaokoa watoto na madhila haya lakini pili tutaweza
kughakikisha kuwa sheria inachukua mkondo wake.

Nilikisikia kisa hiki kutoka kwa watumishi wa UNICEF ambao
wanafanya kazi ya kufundisha makundi mbali mbali hapa
nchini na kwingineko duniani mbinu za kutoa ulinzi kwa
watoto.

Katika wilaya hiyo hiyo ya Hai, UNICEF imesaidia kutoa
mafunzo kwa zaidi ya askari polisi 40. Kwenye kituo cha
polisi cha Boma Ng’ombe, kuna chumba maalumu – cha
hifadhi salama –kwa ajili ya wanawake na watoto wanaofika
kutoa taarifa nyeti za kutendewa ukatili wa aina mbalimbali
pamoja na za kunajisiwa.

Hiki ni kielelezo bora cha ushirikiano baina ya Umoja wa Mataifa na Serikali katika juhudi za kuwalinda watoto dhidi ya ukatili.

Ndiyo sababu tunazindua utafiti huu leo kwenu nyote
wanajamii. Ujumbe wangu mkuu wa leo, ni kwamba, tunazo
takwimu, tunazo tarakimu, hoja si tarakimu na takwimu
nyingi nyingi, ingawa zina umuhimu wake. Bali hoja ni
kwamba, tunayoyazungumza hapa ni madhila halisi
yanayowasibu binadamu halisi kama mimi na wewe,
imetokea kwamba binadamu hao ni watoto wetu, wanyonge.
Tusiruhusu hali hii ya unyonge kwa watoto wetu, kwa hakika
haki zao na usalama wao ni wajibu wetu sisi sote.


Takwimu na taarifa ni muhimu katika kazi zetu,
nimekwishasema hilo, lakini kazi yetu kubwa kabisa ni
kuwalinda watoto wetu, jamii zetu, rafiki zetu na binadamu
wenzetu. Tujue kwamba takwimu hizi zinabeba sura ya mtu
halisi sio takwimu kavu.

Tukishirikiana, na tukisimama pamoja, tunaweza kukomesha
ukatili kwa watoto. Tunaweza kukomesha kabisa vitendo
viovu. Na tunaweza kuwapa watoto wa Tanzania fursa ya
kustawi na kuwa na mustakabali mzuri ambao ni haki yao ya
kuzaliwa.

Nakushukuruni sana kwa kunisikiliza.
Asanteni.

No comments:

Post a Comment