Saturday, November 26, 2011

TAFSIRI YANGU; RAIS KIKWETE KUKUTANA NA CHADEMA:

Ndugu zangu,

WATANZANIA sasa tunakwenda kama mbuzi waliokata kamba. Ukiwafuatilia kwa karibu mbuzi waliokata kamba utawaona wanavyoteseka. Tofauti na mwanadamu, mbuzi wamekosa busara na hekima. Mbuzi waliokata kamba husambaratika na kujiendea bila malengo. Hufika mahali hushindwa kuelewa walikotoka na wanakokwenda.

Yamkini mbuzi waliokata kamba hufika wakiwa wamechoka sana, mwisho wa safari ambayo hawakuipanga wala kuitarajia. Nahofia, tukiendelea kwenda kama mbuzi waliokata kamba, watanzania tutafika mwaka 2015 tukiwa tumechoka sana. Tutangulize sasa busara na hekima. WaTanzania tuna lazima ya kujipanga upya ili tuijenge nchi yetu tuliyozaliwa.

Juzi hapa, kule Dodoma Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete alikaririwa akiyasema haya kwenye NEC ya Chama chake;
“Jamani hapa tunajenga chama, watu wanasubiri kusikia tukimaliza kikao chetu kwa ugomvi, naomba tumalize kwa amani na twendeni tukajenge chama chetu”. ( Mwananchi, Nov 25, 2011)

Hayo ni ya ndani ya CCM. watanzania wengi kwa sasa wanajua kuna mvutano wa kisiasa kati ya CCM na Chadema. Na watanzania hawa wenye kupenda amani na utulivu wangependa kumwona Rais wao Kikwete akikaa meza moja na Chadema. Wanywe chai na kuongea kama watanzania na pengine Rais ayatamke yenye kufanana na ya Dodoma:

“Jamani ndugu zangu wa Chadema, hapa tunajenga nchi yetu, watu wanasubiri kusikia tukimaliza kikao chetu kwa ugomvi, naomba tumalize kwa amani na twendeni tukajenge nchi yetu.”

Naam, watanzania wengi wangependa pia kumsikia Rais wao Kikwete akiyatamka hayo pale atakapoombwa na kukubali kukutana na wawakilishi wa jukwaa la katiba na makundi mengine yenye mawazo tofauti ya namna ya kuendesha mchakato wa kupata Katiba yetu Mpya.

Hata hivyo, watanzania wasingependa, kwa staili hii kuona mjadala wa Katiba unahamia Ikulu na kwa kujadiliwa na makundi teule wakiwa na Rais. Kinachotakiwa ni kutafutwa haraka muafaka ili muswaada huo ulio sasa katika lugha ya Kiswahili urudishwe tena bungeni. Hujadiliwe kwa mara ya kwanza, tutoke huko Bungeni tukiwa na muafaka wa Kitaifa na kutafuta namna ya kwenda mbele.

Ni kwa njia hii ya mazungumzo na kuupata muafaka wa kitaifa ndipo tutaepuka wingi huu wa manung’uniko ambao kimsingi utazaa Katiba ya manung’uniko, itakayotupelekea kwenye uchaguzi wa manung’uniko , utakaozaa matokeo ya manung’uniko. Hivyo basi, tutakuwa tumeandaa Katiba ya kutuletea vurugu katika nchi yetu.

Maana, katika kuongezeka kwa hali ya kukata tamaa na hata kupoteza imani yao kwa CCM na Serikali yao, watanzania wengi kwa sasa wanaiona Katiba Mpya kuwa ni Tumaini Jipya. Tutafanya makosa makubwa kuwaburuza watanzania katika mchakato huu wa Katiba.

Kwa kuitikia kwa haraka na kwa furaha maombi ya Chadema, Rais wetu Kikwete ameonyesha busara na hekima kubwa ya kiuongozi. Hii ni fursa njema katika kufikia muafaka wa Kitaifa. Itasaidia kurudisha imani ya wananchi katika hofu waliyonayo juu ya hatma ya nchi yao. Itasaidia kurudisha imani ya wawekezaji pia. Hivyo basi, inahusu uchumi.

Kuna wakati gari la wagonjwa lilionekana likiingia Ikulu ya Mandela. Taarifa ile ikasambaa haraka na thamani ya Rand, sarafu ya Afrika Kusini ikashuka. Na katika uchumi wa soko mara zote, soko kitabia hushtuka hata kwa hisia tu. Kwamba Rais Mandela mgonjwa soko linahisi haraka kuwa huenda kifo chake kitapelekea machafuko. Ikulu ya Mandela ilipotoa taarifa rasmi kuwa Mzee yuko salama kabisa, basi, soko likawa limetulizwa na Rand nayo ikapanda thamani yake.

Ndio maana ya kuandika, kuwa mazungumzo ya Rais Kikwete na Chadema yanaweza pia kurudisha imani ya wawekezaji tunaowategemea kwa uchumi wetu. Hivyo basi, yumkini picha tu itakayomwonyesha Rais Kikwete akiwa na Freeman Mbowe au Dr Slaa kwenye mazungumzo ya Ikulu na yatakayokuwa yametoa matokeo chanya, yaweza kuchangia kwenye kuimarisha thamani ya shilingi yetu inayoporomoka kwa kasi.

Mimi naamini, kuwa mazungumzo ya Rais Kikwete na Chadema yakiangazia kwa DHATI kwenye maslahi ya nchi yetu, basi, utakuwa ni mwanzo wa ushindi wa watanzania wote. Maana, mazungumzo yatakayozingatia kwa DHATI maslahi ya nchi yetu yatampelekea Rais wetu kusitisha uamuzi wake wa kusaini muswaada wa Sheria ya Mchakato wa Katiba, kitu ambacho hata mimi ningeombwa mawazo yangu, ningeshauri hivyo, kwa maslahi ya Tanzania.

Na kwa hakika, Rais Kikwete akionyesha subira na utayari wa kupisha njia ya majadiliano na hatimaye kufikiwa muafaka wa Kitaifa wa namna ya kwenda mbele, basi, katika mambo atakayokumbukwa nayo hata baada ya Urais wake, hilo litakuwa jambo kubwa kabisa na jema atakalokumbukwa kuwatendea watanzania.

Tunajua, kuwa katika uitikio huu wa Rais Kikwete kukutana na Chadema, kuna wenzake ‘ wahafidhina’ ndani ya CCM wasiofurahishwa na hatua hii. Wameanza kazi ya kuweka magogo kwenye barabara ya kwenda kwenye muafaka wa kitaifa kuhusu Katiba. Historia ni mwalimu mzuri, hayo yalitokea Zanzibar pia wakati wa mgogoro wa CCM na CUF.

Tumeona, badala ya kumpongeza Rais na kumuunga mkono, zinatia mashaka, kauli hizi za Kamati Kuu ya CCM ‘ kumwagiza’ Rais Kikwete awajumuishe pia wapinzani wengine kwenye meza hiyo ya mazungumzo ilihali wakijua kuwa ni Chadema walioonyesha heshima ya kumwandikia barua Rais kukutana kuongea nae. Hivyo basi, Chadema wametambua uwepo na umuhimu wa Kikwete kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ndio, Wahafidhina hao ndani ya CCM ambao miongoni mwao fikra zao haziko kwenye Tanzania ya miaka 50 ijayo bali ziko kwenye mikakati ya Urais wa 2015, wanajua pia, kuwa Augustino Mrema Wa TLP na Hamad Rashid wa CUF licha tu vyama vyao havikuomba kukutana na Rais, pale bungeni walisimama ‘ kuwazodoa’ Chadema na kuunga mkono kwa asilimia mia moja muswaada ule wa sheria ya Katiba. Sasa waheshimiwa hawa, Mrema na Hamad, kwenye meza ya mazungumzo pale Ikulu ya Magogoni wakakae upande gani?

Wahenga wetu walisema; yalopita si ndwele, tugange yajayo. Ni wakati sasa wa kuitumia fursa iliyojitokeza ili tuutafute muafaka wa Kitaifa. Ndio, twende mbele kama taifa hata kama tunatofautiana kifikra. Tuanze sasa kuachana na dhana ya kuongozwa na ilani za vyama. Tutengeneze kwa pamoja Ajenda ya Taifa. Ajenda ya Taifa ni Ndoto Ya Taifa. Katiba Mpya itakayowashirikisha WaTanzania katika hatua zote itatusaidia kuifikia ndoto hiyo. Inawezekana.


Mungu Ibariki Afrika,

Mungu Ibariki Tanzania.
Maggid Mjengwa,
Dar es Salaam.
Ijumaa, Novemba 25, 2011

No comments:

Post a Comment