Thursday, December 15, 2011

KAMANDA LEMA ANACHANJA MBUGA KWENYE VITA YA MTANDAONI:

Ndugu zangu,

Zimebaki takribani saa 26 kabla ya vituo vya kupigia kura kufungwa. Ni  kwenye Pima- Maji ya
www.mjengwablog.com  .  Anga ya mtandaoni  imechafuka kwa vita kali ya kuwania kura. Ni vita ya usiku na mchana. Ni katika mchakato huu wa kumpata mbunge bora Kijana kwa mwaka 2011.
Habari kubwa siku ya leo?

Ni ’ Kamanda’  Godbless Lema.

Mtu huyu Godbless Lema anaonekana kuwa jeshi kubwa la ’Wanamgambo wa mtandaoni’. Alfajiri  hii ninapoandika uchambuzi huu mfupi,  ’ Kamanda’ Lema, kama anavyoitwa na wafuasi wake anaongoza kwa  kura  zaidi ya mia mbili. Lema  yuko  mbele ya Zitto Kabwe huku akiwa  amemwacha nyuma John Mnyika aliye nafasi ya tatu kwa kura zaidi ya elfu moja na m ia sita. Naam, vita kali kwa sasa ni kati ya   Godbless Lema na Zitto Kabwe.

Ilivyo sasa:

Kura zipatazo elfu na mia sita  zitakuwa zimepigwa kwa siku ya kupiga kura itakayomalizika muda mfupi ujao.  Ni ongezeko la kura mi sita kutoka idadi ya kura zilizopigwa jana.  Kura 1600 kwa siku, ni rekodi mpya!

Tafsiri yake?

Kura hizi za mtandaoni ambazo mwanzoni kuna waliojitokeza na kuzibeza kwa nguvu zote zinazonekana kuwavutia wengi na kuwa ni kipimo kinachokubalika kisayansi katika kupima ’kina cha  maji ya kisiasa’ ama upepo wa kisiasa kama inavyofahamika na wengi.

Ndio maana tumeona, kuwa kura hizi za mtandaoni  zimeamsha hamasa ya kisiasa kwa vijana, dada na kaka zao katika siasa  na nje ya siasa,  na hata wazee pia, walio ndani na nje ya siasa.  Naam, kwa anayetaka kujifunza, basi, kuna mengi ya kujifunza katika kufuatilia mwenendo wa kura hizi.

Zitto Kabwe:
Yuko nyuma  ya Lema kwa kura mia mbili.

Zitto Kabwe anazijua  njia za kupita mtandaoni na kukusanya kura. Ameonyesha uwezo wa kukusanya kura zaidi ya mia moja za mtandaoni ndani ya dakika 80. Hivyo basi, Lema anayeongoza kwa kura mia mbili hawezi  na hapaswi kujiamini. Kwamba yaweza kuwa makosa kwa Lema   kusimama njiani na kuanza kunywa  juisi kabla kipenga cha  mwisho wa kupiga kura kupulizwa.

 Kulikoni Kijana John Mnyika ?
Bado yuko kwenye nafasi ya tatu. Ameacha nyuma na  Zitto kwa zaidi ya kura elfu moja. Kwa Mnyika kupanda kwenda nafasi ya pili ni jambo lisilowezekana kwa sasa. Na kushuka toka alipo kwenye nafasi ya tatu nako hakuwezekani. Hivyo basi, John Mnyika atabaki kufuatilia na kutafsiri mtanange unaoendelea sasa kati ya Zitto na Lema.

Mr. Sugu ’kajituliza kwake kasuku?’
” Hapendi matata, hapendi maneno!”  Sugu, kama nilivyomwelezea juzi, anaelekea kwenda kugota kwenye kura mia na kitu, na si zaidi.  Lakini, ni muhimu naye  akaanza kutambua, kuwa mapambano ya kisiasa huko tunakokwenda yatahitaji pia juhudi na uwezo wa kupambana mtandaoni.

January Makamba: 
Pamoja na kuwa wa kwanza kutamka kuwa kura hizi si za Kisayansi, namwona ndugu yangu January Makamba akiwa amekaa na kalamu na karatasi. Anachambua ’ Kisayansi’ mwenendo wa kura hizi na tafsiri yake katika juhudi za kulikamata kisiasa na ’ Kisayansi’ kundi la vijana.  January Makamba amebaki na kura tatu kufikisha kura mia moja. Yawezekana.

’Mo’ Dewji
Ni mtu wa mikakati. Katika ’ biashara’ ya siasa ’ Mo’ Dewji ataangalia kwanza faida aliyoipata katika mchakato huu; kuwa ametambulishwa hata kwa wale ambao hawakumfahamu sana kisiasa. Na biashara ya siasa ni kujitangaza kama ilivyo biashara nyingine. Hilo la mwisho ’ Mo’ Dewji hahitaji kwenda darasani. Maana, anajua pia, kuwa ’ Kiduku’ kimempandisha chati pia!
 Mkosamali kakumbuka shuka kumekucha!
  Katika siku mbili hizi Mkosamali kafikisha kura sita kutoka kura mbili. Anamzidi  Peter Serukamba kwa kura tatu.  Katika mchakato huu kuna ’ Ligi’ zaidi ya moja.
Naam, siku ya leo nayo inaweza ikazaa habari mpya kesho. Nenda sasa www.mjengwablog.com kupiga kura yako. Mahali ni juu kulia.

Maggid Mjengwa,


Mratibu.
Iringa
Lakini, kwa mtu makini ataweka kichwani, kuwa ” You Should Never  Count Him Out!”- Kwamba kwenye karata za kisiasa, kamwe usimtoe  Zitto Kabwe kwenye hesabu zako. Niliandika juzi, kuwa Zitto Kabwe ni mwanasiasa kijana lakini mkongwe mtandaoni na hata nje ya mitandao. Ana uzoefu wa uwanja wa mapambano.

No comments:

Post a Comment