Sunday, October 30, 2011

MHESHIMIWA ZITTO KABWE ANAENDELEA VYEMA NA MATIBABU NCHINI INDIA, ATUMA SALAMU ZA SHUKRANI:

Mbunge wa Kigoma Kaskazini Mheshimiwa Zitto Kabwe.

Ndugu zangu,
Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuniwezesha muda huu kuwa na nguvu za kukaa katika kiti na kuweza kuandika haya machache kwenu. Nawashukuru sana Wanamabadiliko kwa salaam zenu nyingi za pole mara mliposikia ninaumwa na kulazwa hospitalini. Najua hamkuwa na taarifa kamili za kuumwa kwangu na kwa kweli suala la kuumwa ni suala la mtu binafsi (hata kwa mtu mwenye dhamana ya kiuongozi wa umma japo umma nao una haki ya kujua kinachomsibu kiongozi husika).
Mwanzo
Nilianza kupatwa na maumivu ya kichwa usiku wa siku ya Ijumaa tarehe 20 jijini Dar es Salaam mara baada ya kuwasili kutoka Jimboni tayari kwa kazi za Kamati za Bunge ambapo Kamati yangu ilikuwa imekwishaanza kazi wiki hiyo kwa kupitia mahesabu na utendaji wa Mamlaka za Maji nchini. Kama kawaida yangu niliona maumivu hayo makali kama ni sehemu tu ya uchovu wa ziara za Jimboni na safari za mara kwa mara nilizofanya kuinigilia ziara za Jimboni ikiwemo kuhudhuria Mdahalo wa Umeme na Mkutano wa Uwekezaji Kanda ya Ziwa Tanganyika. Hivyo nililala na nilipoamka kichwa kilikuwa kimepona na hivyo nikahudhuria kikao cha Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma katika Ofisi ya Bunge mpaka saa saba mchana.
 

Siku ya Jumapili saa kumi na moja jioni nikiwa katika Hoteli ya Southernsun nilipatwa na homa kali ghafla. Nilikatisha mkutano niliokuwa nao na kuamua kurejea nyumbani, lakini nilishindwa kuendesha gari na hivyo kumwomba Dereva wa Mhe. Mhonga anifuate ili anisadie kunifikisha nyumbani. Nilipofika nyumbani kwangu Tabata, homa ilizidi kupanda na hivyo kuamua kwenda Hospitali mara moja. Nikapelekwa Agakhan Hospital na nikapata huduma. Nilipochukuliwa vipimo ilionekana sina malaria wala homa ya matumbo na pia hawakuweza kuona sababu ya homa ile namna ile (maana ilifikia degree 40). 
Walituliza homa, nikapewa Panadol na baadaye nikaruhusiwa kurudi nyumbani mnamo saa tano usiku. Nilipoamka siku ya Jumatatu nikaenda kazini kuongoza Kikao cha Kamati ya Bunge ambapo tulikuwa tunashughulikia Hesabu za Bodi ya Utalii na Benki ya Posta Tanzania. Nilipita Agakhan kupata majibu ya ziada na kuambiwa nipo sawa ila nipumzike nisifanye kazi kwa siku kadhaa na nitakuwa sawa.
Hali kubadilika
Siku ya Jumanne niliamka nikiwa salama, kichwa kikiuma kwa mbali lakini sio vya kutisha. Nikawajulisha wajumbe wenzangu wa kamati kuwa sitakwenda kazini na wao waendelee na kazi. Hata hivyo ilipofika saa sita kamili nilianza kutetemeka mwili mzima na homa kuwa kali sana huku kicha kikiniuma sana sana sana! Dada zangu wakamwita Driver na kunikimbiza Hospitali ya Agakhan. Wakarejea vipimo vilevile na matokeo yakawa yaleyale. Joto lilifika degree 39.8 Hivyo wakanipa dawa za kupoza homa na maumivu ya kichwa kwa drips na sindano kadhaa. Siku ya pili hospitalini nikafanya vipimo zaidi ikiwemo ultra sound na vyote kuonekana sina tatizo lolote. Niliendelea kuwepo Hospitali na kwa kweli hali ilikuwa inatia moyo sana kwani nilipata nguvu na hata kuweza kuzungumza, homa ilikuwa imepungua sana. Pamoja na kwamba Mganga Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na Waziri wa Masuala ya Bunge na Daktari wangu binafsi kuwataka waangalie upya vipimo vya malaria, madaktari wa Agakhan waliwahakikishia viongozi hawa na Daktari wangu kwamba hawajaona Malaria na hivyo wanaendelea na uchunguzi wa 'a trigger' ya homa kali niliyokuwa napata.
Hali kuwa Mbaya
Usiku wa siku ya Jumatano Hali ilikuwa mbaya sana. Joto lilipanda tena kufikia 40 na kichwa kuuma zaidi. Nilikuwa kama ninatwangwa kwenye kinu kwa kweli. Nilikuwa natetemeka sana. Ilikuwa taharuki kubwa sana katika chumba nilicholazwa. Wageni waliokuwa wamekuja kunijulia hali wakati hali inabadilika ilikuwa ni pamoja na Ndugu Murtaza Mangungu na Mohamad Chombo ambao ni wajumbe wa Kamati ya Bunge ya POAC, walishauri mara moja nihamishwe Hospitali kupelekwa Muhimbili. Muda si mrefu kupita Waziri Lukuvi na Katibu wa Bunge walifika, wakaafiki na nikahamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili na kwa hali niliyokuwa nayo nikalazwa katika Chumba wanachokiita Mini-ICU. Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Mama Blandina Nyoni alikuwepo Hospitalini tayari.

 
Usiku huo huo nilifanyiwa vipimo upya. Full Blood picture pamoja na BS. Vile vile kufuatia malalamiko kuhusu maumivu ya kichwa ikaamuliwa kuwa nifanyiwe CT Scan usiku ule. Ikaonekana nina wadudu wa Malaria 150 na mara moja nikaanza matibabu. Namshukuru sana Daktari kijana Dkt. Juma Mfinanga kwa umahiri mkubwa aliouonyesha tangu nilipofika pale Mini ICU. Asubuhi ya siku ya pili nikapata majibu ya tatizo la maumivu ya kichwa. Nimekuwa nasumbuliwa na kichwa kwa miaka zaidi ya Kumi sasa na katika kipindi hicho mara nne nilipoteza fahamu na kuanguka (Mara ya kwanza mwaka 2000 nikiwa Jijini Mwanza nikielekea kwenye Mkutano wa Vijana wa National Youth Forum, Mara Pili Mjini Dodoma katika mkutano kama huo mwaka 2001 lakini ilikuwa usiku,Mara ya tatu Nikiwa chumbani, Hall II mara baada ya kutoka  Prep, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2002 na mara ya Nne Bungeni siku ya kupitisha Muswada wa Madini 2010 kufuatia wiki nzima ya Kamati na Mjadala wa Bunge(Ndugu Katulanda anakumbuka siku hii kwani yeye ndiye niliyemkamata njiani kunikimbiza Zahanati ya Bunge).

Tatizo lililogundulika ni SINUSITIS, ambayo tayari imekuwa sugu. Daktari Bingwa wa magonjwa haya Dkt. Kimaryo akanieleza kwa kirefu juu ya tatizo hili na kuniambia suluhisho ni 'surgery' na pale Hospitali ya Taifa hawafanyi hiyo operesheni. Akashauri niletwe India ambapo kuna Daktari mpasuaji wa ugonjwa huu. Nikakubali.

Baada ya kuwa Malaria imedhibitiwa kwa kufikia nusu ya 'dozi' nilopewa na wadudu kuonekana kutokomea, Ofisi ya Bunge ikaandaa safari. Nimefika India. Nimebakiza sindano mbili ili kumaliza 'dozi' hiyo na tayari nimefanyiwa taratibu zote kwa ajili ya 'surgery' hiyo.
Sijafa
Uvumi ulienezwa nimekufa. Kwa kupitia kwenu ndugu zangu WanaMabadiliko, napenda Watanzania wenzangu wajue mimi ni mzima wa Afya. Nimepata maradhi kama Binadamu mwingine yeyote anavyoweza kupata na namshukuru Mungu kwamba ninapata matibabu mazuri kabisa.
Shukrani
Nawashukuru sana Madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili chini ya Prof, Mwafongo kwa juhudi kubwa walioonyesha katika kunihudumia.Naishukuru Ofisi ya Bunge kwa Kutimiza wajibu wao kwangu kama Mbunge,Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya kwa kuonyesha upendo wa hali ya juu na watumishi wote wa Wizara ya Afya, Katibu Mkuu wa CHADEMA Dkt. Slaa kwa ufuatiliaji wa karibu wa Afya ya Naibu wake, Wabunge wajumbe wa Kamati ya POAC, Dkt. Alex Kitumo,ndugu, jamaa na marafiki zangu wote.Nawapa pole wananchi wa Jimbo la Kigoma Kaskazini kwa uvumilivu mkubwa hasa kufuatia uvumi mbalimbali ulioenezwa, pia Watanzania wengine kwa uzito huo huo.

Nitawajulisha kwa lolote Mungu akipenda. Ninaendelea na matibabu na hali yangu ni nzuri
Ndugu yenu.

Zitto.

Kabwe Z. Zitto, MP- Kigoma North, Tanzania.
Chairman Parliamentary Public Investments Accounts Committee (POAC),
Deputy Secretary General CHADEMA and Deputy Leader of the Opposition,
Shadow Minister of Finance
Mobile: +255756809535
Blog: http://www.zittokabwe.com/

No comments:

Post a Comment