Thursday, October 18, 2012

MWENYEKITI WA JUMUIYA YA MADAKTARI TANZANIA (MAT), DK STEPHEN ULIMBOKA, ATOA TAMKO BAADA YA KIMYA KIREFU:

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Stephen Ulimboka, akisaini tamko lake kwa watanzania ambalo lilisomwa kwa niaba yake na Wakili wake, Nyaronyo Kicheere, Dar es Salaam. Kulia ni Wakili na Kamishna wa Viapo, Rugemeleza Nshala. Tamko hilo alisaini Oktoba 07, jijini Dar es Salaam.Picha na Joseph Senga
--
HATIMAYE Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Stephen Ulimboka, amefunguka na kudai maelezo yote aliyoyatoa na kurekodiwa kabla na baada ya kufika hospitali ni ya kweli.

Alisema alitoa maelezo hayo, akiwa na kumbukumbu sahihi na kuwataka Watanzania, kupuuza wale wote wanaotaka kupotosha ukweli juu ya tukio hilo.

Akisoma tamko hilo, kwa niaba ya Dk. Ulimboka, Wakili wa kujitegemea Nyaronyo Kicheere alisema, amepewa jukumu la kuwasilisha tamko hilo, kwa Watanzania kwa kuwa, Dk. Ulimboka yuko nje ya nchi akiendelea na matibabu yake aliyoanza mapema, baada ya kutekwa na kuteswa na watu wasiojulikana.
Pamoja na mambo mengine, Dk. Ulimboka amedai yuko tayari kuhojiwa na kutoa ushirikiano kwa vyombo huru na makini vya uchunguzi, ambavyo vitaundwa ili kuweza kubaini ukweli.

Akisisitiza uthibitisho wa madai hayo, Dk. Ulimboka alisema, maelezo aliyoyatoa ambayo yamerekodiwa kwenye mtandao wa You Tube, ni ya kweli na wakati anatoa maelezo hayo, alikuwa na kumbukumbu nzuri bila athari yoyote pamoja na maumivu makali.

“Uthibitisho wa kumbukumbu nzuri, niliyokuwa nayo ni pale nilipokutana na Juma Mganza, katika msitu wa Mabwepande asubuhi ya siku ya tukio, pamoja na maumivu makali niliyokuwa nayo kila sehemu ya mwili wangu, niliweza kumshawishi Mganza anifungue kamba za mikono nilizokuwa nimefungwa…pia kukumbuka namba ya simu ya rafiki yangu Dk.Deogratius, ambapo Mgaza aliweza kuwasiliana naye kumpa taarifa ya tukio hilo na mimi kufikishwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.

“Najua wapo watu ambao wamekuwa wakihaha kupindisha ukweli, lakini wanasahau kuwa, niliweza kumshawishi Mganza hadi akashawishika kunikaribia na kunisikiliza pamoja na hofu aliyokuwa nayo ya kukutana na mtu aliyekuwa katika hali kama yangu.

Niliweza kukumbuka namba ya rafiki yangu, mambo hayo yanatosha kuthibitisha nilichokisema ni ukweli na kuwa, utimamu na kumbukumbu zangu ni sahihi,” alisema Dk. Ulimboka katika tamko hilo.
Akizungumzia tukio la kutekwa na kuteswa kwake kabla halijatokea, alisema alikuwa na kikao na afisa wa Ikulu, Ramadhani Abeid Ighondu.

“Nathibitisha kuwa, Ighondu alitambulishwa kwetu kwa jina la Abeid na kigogo mmoja, binafsi ninamfahamu sana huyu kwa sababu alikuwa akitumwa mara kwa mara kuja kukutana na mimi na tumekutana mara kadhaa kabla ya tukio lile.

“Tulitambulishwa kwake mimi na madaktari wenzangu, kuwa yeye ndiye atakayehusika kuchukua madai na hoja za madaktari katika mgogoro wetu na Serikali, nathibitisha kuwa, mfanyakazi huyu wa Ikulu, ndiye aliyenipigia simu ambapo alikuwa akitumia namba (tunayo) na kuniita kwenye kikao ambapo muda mfupi baadaye nilitekwa.

“Hakuna shaka, namtambua Abeid kwa sura na naamini kwa dhati kuwa, afisa huyu bado yuko hai… mimi na wenzangu tuko tayari kutoa ushirikiano kwa chombo huru kuhakikisha haki inatendeka.
“Naendelea kuthibitisha kuwa, Abeid ninamfahamu na hata akikamatwa leo hii nitakwenda kufanya utambuzi, ninasikitika hatujasikia popote kuwa, Abeid pamoja na washirika wake wamehojiwa pamoja na jamaa waliotajwa mpaka sasa.

“Ninafahamu kuwa, ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inatoa kinga kwa uhai wa kila mtu anayeishi katika nchi yetu, tena inaitaka jamii kulinda uhai wa kila mtu, mimi Ulimboka Stephen, ninafahamu kwamba nina haki ya kuishi na kuwa Serikali yangu na wananchi wenzangu, wanajukumu la kuulinda uhai wangu.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu kwa nini Dk. Ulimboka amemchagua yeye kuwasilisha tamko hilo, Wakili Kicheere alisema, imani yake kwake ndiyo iliyopelekea yeye kupewa madaraka hayo.
Wakili Nyaronyo alitoa tamko hilo, kwa usimamizi wa mwanasheria Rugemeleza Nshala, Oktoba 14, mwaka huu ili aliwasilishe kwa Watanzania, lakini siku zote hizo alikosa ukumbi hadi jana alipopata nafasi katika ofisi za Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRD).

Dk. Ulimboka alitekwa usiku wa Julai 26, mwaka huu na watu wasiojulikana, ambapo aliteswa na kunyofolewa kuacha na kung’olewa meno na baada ya hapo alisafirishwa kwenda nchini Afrika Kusini.

No comments:

Post a Comment