Monday, February 6, 2012

JINSI NYAMONGO KULIVYOLIPUKA, POLISI WAUWA MMOJA:

MKAZI wa kijiji cha Nyarwana, kata ya Kibasuka, tarafa ya Inchage wilayani hapa, Daniel Masimbe ameuawa na polisi kwa kupigwa risasi baada ya kuvamia mgodi wa dhahabu wa North Mara - Nyamongo.
Masimbe (20) alikufa papo hapo baada ya risasi hiyo kumpiga koromeo na kutokea mgongoni dakika chache baada ya kuvamia mgodi huo juzi.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Tarime/Rorya, Sebastian Zakaria alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea saa 6.30 mchana, baada ya kundi la watu zaidi ya 100 wenye silaha za jadi yakiwamo mapanga, marungu na mawe, kuvamia kwa lengo la kupora mawe ya dhahabu.

“Watu hao wengine wakiwa ndani ya mgodi na wengine nje, walizua tafrani wakitaka kupora mawe na askari wetu walijaribu kuwazuia kwa mabomu ya kutoa machozi bila mafanikio na baada ya kuona watu hao wanawazingira, walitumia risasi za moto ili kujiokoa na kuzuia uhalifu mkubwa zaidi,” alisema.

Kamanda Zakaria alisema Masimbe ambaye alikuwa mstari wa mbele wa uvamizi huo, alipigwa risasi kwenye koromeo ikatokea mgongoni na kumuua papo hapo. “Polisi walipambana na kundi hilo hadi kuzima uvamizi huo na kulitawanya,” alisema Kamanda Zakaria.

Alisema mwili wa marehemu ulipelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime na kufanyiwa uchunguzi kabla ya kuchukuliwa na ndugu zake kwa ajili ya maziko kijijini kwao Nyarwana.
Kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi limewaonya wananchi kuacha kujihusisha na vitendo vya uhalifu hasa kuvamia mgodi huo, kwa vile mwekezaji yupo hapo kihalali na analindwa na sheria za nchi.

Hii ni mara ya pili katika kipindi cha miezi tisa, kwa Polisi kukabiliana na wavamizi katika mgodi huo na kuwaua. Mei mwaka jana, polisi waliua watu watano kwa risasi na kujeruhi wengine sita baada ya watu 800 kuvamia mgodi huo wa Nyamongo, wilayani, Tarime.
Watu hao walivamia mgodi huo kwa lengo la kuchukua mchanga wa dhahabu na kupambana na polisi wanaolinda mgodi huo.

Kamanda wa wakati huo, Costantine Massawe alisema tukio hilo lilitokea katika eneo la kinu cha dhahabu, ambapo watu wanaokadiriwa kuwa kati ya 800 na 1,000, wenye silaha za jadi yakiwamo makombeo, walivamia eneo hilo ili wachukue mchanga huo.

Waliouawa walikuwa Chacha Ngoko (25), mkazi wa Kewanja Nyamongo, Emmanuel Magige Ghati (19), mkazi wa kijiji cha Nyakunguru, Chacha Mwasi (23) wa kijiji cha Bisarwi Komaswa na wengine wawili ambao majina yao hayakutambuliwa mara moja.

Katika tukio hilo, polisi wawili Mkuu wa Kituo cha Tarime Hassan Mayaa alipigwa jiwe kichwani na kujeruhiwa na Mrakibu Msaidizi wa Polisi Simon Mrashani naye alijeruhiwa kiunoni kwa kupigwa jiwe.

No comments:

Post a Comment