Sunday, July 31, 2011

MAREKEBISHO YA SHERIA YA KUDHIBITI MAANDAMANO YAJA:


Jaji Fredrick Werema (Kulia).
Akichangia hotuba hiyo juzi kabla ya kuahirishwa kwa Bunge kwa ajili ya mapumziko, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema alisema mabadiliko hayo ya sheria yatalenga kuzuia bughudha katika maeneo ambayo watu hawashiriki maandamano husika.

Maandamano ni miongoni mwa mambo ambayo yalitawala mjadala wa siku mbili bungeni wa hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, iliyowasilishwa hivi majuzi na Waziri Shamsi Vuai Nahodha

"Tunadhani kuna haja ya kurekebisha sheria ili kuregulate (kudhibiti) maandamano katika maeneo ambayo watu si washiriki wa maandamano hayo, hili linawezekana maana nchi kama Ujerumani wamefanya hili," alisema Werema na kuongeza:

"Nimesikia hapa kauli mbalimbali zinazohamasisha maandamano na wengine wanasema tutaandamana mpaka kieleweke na wengine wanasema kutoka Mwanza mpaka Dar es Salaam, tunasema ndiyo ni haki ya kisheria, lakini lazima tuzingatie kwamba wapo wasiopenda maandamano haya."

Kadhalika, Werema alitumia nafasi hiyo kutoa somo kwa wabunge kuhusu mivutano iliyotokea bungeni siku chache zilizopita: “Peaneni nafasi kwa kila mtu na mwenzake na muwe na ushirikiano kama ambavyo mikono ya kushoto na kulia inakuwa na ushirikiano mzuri.”

Jaji Werema aliwaambia wabunge kuwa kazi ya kuwakilisha wananchi inahitaji uvumilivu kuliko kazi nyingine na akawataka wabunge wa pande zote kutumia lugha za kistaarabu wanapo kuwa ndani ya ukumbi wa bunge.

Hata hivyo, alikemea tabia za baadhi ya wabunge kutumia lugha za maneno makali akitolea mfano wa hotuba ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani Bungeni kuhusu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi... “Ni kweli Mheshimiwa Lema (Godbless) alitumia lugha kali kidogo.

Hapa naomba ifahamike hivyo, lakini yote mimi ambaye ni Mwanasheria wa Serikali nasema muendelee kuvumiliana na kuangalia lugha za kutumia. Namshukuru sana Mheshimiwa Lukuvi (William), katika hotuba ile alitaka kusimama amzuie Lema, lakini nikamwabia muache aendelee kwani kuna njia nyingi za kuzungumzia hivyo akimaliza utaomba mwongozo.’’

Alisema kuwa katika suala lile yeye (Werema) akiwa Mwanasheria Mkuu, ndiye mwenye dhamana ya kulisemea jambo hilo.

Habari hii ni hisani ya tovuti ya mwananchi, Zaidi, tembelea: http://www.mwananchi.co.tz/

No comments:

Post a Comment