Sunday, May 26, 2013

KELELE ZA GERARD PIQUE NDANI YA MFULULIZO WA MAKALA ZA "MLALAMISHI"


Kuanzia leo, tutakuwa tukiwaletea mfululizo wa makala za MLALAMISHI ambazo zitalenga kuchambua matukio mbalimbali katika viwanja vya michezo tofauti tofauti. makala hizi zitalenga kuonesha upande wa pili wa matukio ambaye yameripotiwa kwa kiasi kikubwa upande mmoja tu.. Leo tutaanza na malalamiko ya Gerard Pique wa FC barcelona aliyoyatoa kufuatia wiki mbaya ya vipigo viwili mfululizo vya El Classico.



Msimu wa 82 wa ligi kuu nchini Hispania, Liga BBVA- zamani La Liga, uko katika hatua za mwisho huku FC Barcelona wakiwa wamekwishajihakikishia ubingwa wao wa 22. Kama kawaida ya soka la Hispania kwa misimu kadhaa sasa, ligi ya msimu huu ilikuwa sawa na mbio za farasi wawili kati ya Real Madrid na FC Barcelona. Atletico Madrid walijitahidi kufukazana na wababe hawa wawili lakini baadaye wakaishiwa pumzi na kusalimu amri. 

Kuna mambo na matukio mengi yaliyoacha kumbukumbu ndani ya msimu huu; mgogoro wa ndani kwa ndani wa Real Madrid, Maradhi ya kansa kwa kocha wa FC Barcelona-Tito Vilanova na matatizo ya kiutawala na kifedha ya klabu ya Malaga  ni baadhi ya mambo hayo. Lakini tukio ambalo ningependa kulichambua leo ni  malalamiko ya mlinzi wa FC Barcelona, Gerard Pique, aliyoyatoa mara tu baada ya Barcelona kupoteza mechi ya El Clasico ya La Liga ya Jumamosi ya March 2, 2013. Mlinzi huyo wa kati wa miamba hao wa Katalunya, Gerard Pique, alimtupia lawama mwamuzi  Miguel  Angel Perez Lasa  kwa kuipendelea Real Madrid. Pique aliamini Barcelona hawakustahili kupoteza mechi ile kama wangepewa “penati ya wazi” dakika za mwisho za mchezo pale Sergio Ramos alipoonekana kumuangusha Adriano.

Pique alisikika akisema, “tunajua mambo haya yanavyokuwa. Unapocheza dhidi ya Madrid, kama matokeo yanalingana chochote kinaweza kutokea. Kama ilivyotokea, haikutokea kwa upande wetu. Kama mwamuzi anaingia mchezoni, lazima tupoteze” Akaongeza, “nafikiri hakuiona ile penati na natumaini safari ijayo ‘atatuua’ tena na ataomba radhi”.


 ‘Penati’ iliyomnyima usingizi Gerard Pique. Bila shaka itamyima usingizi mwaka mzima.


Pique alikuwa akilalamikia penati ambayo kama Barcelona wangepewa na kufunga basi wasingepoteza mchezo wa pili mfululizo kwa Real Madrid, mpinzani wao mkubwa kihistoria, kisoka, kiutamaduni na kisiasa. Pique kama mkatalunya halisi,kama walivyo wakalunya wote, hakuna kitu ambacho anakichukia zaidi ya Madrid kama timu na kama mji (au jimbo kabisa)

Real Madrid na Barcelona ni timu zenye upinzani wa kihistoria. Upinzani wa timu hizi ni wa kurithi kutoka majimbo zinakotoka timu zenyewe. Real Madrid inatoka jimbo la Castilla na Barcelona inatoka jimbo la Katalunya( Catalan). Wakati wa utawala  wa kidikteta wa Miguel Primo de Rivera, aliyekuwa waziri mkuu wa Hispania kuanzia 1939–1975 na General  Francisco Franco aliyekuwa mkuu wa majeshi kuanzia mwaka 1936 mpaka  1975, lugha zote za majimbo (kikiwemo kihispniola cha kikatalunya) zilipigwa marufuku nchini Hispania na Lugha pekee iliyokuwa rasmi ilikuwa Castillian, kihispaniola kinachotumika Madrid (ambako watawala walikuwa wanatoka). Katika kipindi hiki hata jina la klabu yao lilibadilishwa kutoka FC Barcelona ( Football Club Barcelona) na kuwa Barcelona CF (Barcelona Club de Futbol) kwa sababu FC Barcelona limekaa kiingereza sana, Barcelona CF ni kihispniola japo maana ni moja.

Hali hii iliwafanya watu wa Katalunya kuuchukia utawala mzima wa Hispania na kutaka kujitenga , na wakaona njia nyepesi ya kuupinga utawala wa Madrid ni kujiunga na klabu ya Barcelona. Mwaka 1925 walizomea wakati wimbo wa taifa unapigwa na kupelekea uwanja wao wa  Camp de Les Corts kufungiwa kwa miezi sita, kwao hii ndio ilikuwa njia pekee ya kuonesha hasira zao  kwa sababu harakati nyingine zozote zilipigwa marufuku na zilikuwa hatari sana kwa maisha yao. Ndio maana kwa watu wa Katalunya, Barcelona ni Més que un club (zaidi ya klabu) na maneno hayo utayakuta ndani ya uwanja wa Nou Camp.

Pique alikuwa akilalamikia penati ambayo kama Barcelona wangepewa na kufunga,  basi wasingepoteza mchezo wa pili mfululizo kwa Real Madrid ya Jose Mourinho, kocha ambaye wakatalunya hawamkubali kama mtaalamu wa soka bali mtaalamu wa lugha; mkalimani!

Katika safari yake ya kuwa ‘Special One’, Jose Mourinho, alipitia Nou Camp kuanzia mwaka 1996 mpaka 2000 kama mkalimani wa Sir Bobby Robson, aliyekuwa kocha wa FC Barcelona. Kwa kuwa Mourinho alikuwa na diploma ya sayansi ya michezo kutoka chuo kikuu cha Lisbon, Robson aliamua kumtumia pia kama msaidizi wake. Robson alikuwa na mbinu nzuri za kushambulia na Mourinho alikuwa na mbinu nzuri za ulinzi na muunganiko wao uliisaidia FC Barcelona kutwaa kombe la washindi la ulaya mwaka huo (kombe hili , mwaka 1998/99,  liliunganishwa na kombe la UEFA ambalo sasa ni Europa League).

Msimu mmoja baadaye Sir Bobby Robson aliondoka FC Barcelona, lakini wakuu wa FC Barcelona walimtaka Mourinho aendelee kubaki ili awe msaidizi wa kocha wao mpya Louis van Gaal . Muunganiko wa mtaalamu Van Gaal na Mourinhouliiisaidia  FC Barcelona kushinda La Liga mara mbili mfululizo. Van Gaal alimkubali sana Mourinho na kuna wakati alimuachia majukumu ya  kikosi cha kwanza kwenye baadhi ya makombe na yeye (Van Gaal ) kuwa kama msaidizi wake ili kumjenga na kumkomaza. Kupitia mpango huo, FC Barcelona ilishinda ubingwa wa Katalunya mwaka 2000. Lakini licha ya mafanikio yote  hayo, wakatalunya hawataki kumkubali Mourinho kama alikuwa kocha pale kwao bali mkalimani tu.

Ukichanganya chuki hizi utaona ni kiasi gani Pique aliumizwa na penati ile. Nasema ni chuki tu kwa sababu hata kama FC Barcelona wangepewa penati ile na kufunga na kufanya mchezo uwe sare, isingewaongezea kitu kikubwa kwenye kiti cha usukani wa la Liga na hata kufungwa kwao hakukuwaathiri kiasi kikubwa kwenye kampeni yao ya kuwania ubingwa wao wa 22 wa La Liga.
Mpaka mechi ile Barcelona walikuwa wanaongoza ligi kwa pointi 12 juu ya Atletico Madrid aliyeko nafasi ya pili.

Pique anatuambia waamuzi wanaipendelea sana Real Madrid. Lakini kiukweli kama kuna timu ambayo inafaidika na maamuzi mabovu ya wapuliza vipyenga, basi FC Barcelona ya Gerard Pique inaongoza. Tuanzie kuangalia takwimu kuanzia msimu wa 2008-09 ambao yeye Pique alirudi ‘nyumbani’ Nou camp kutoka ‘uhamishoni’ Old Trafford.

Msimu huo wa 2008-2009, FC Barcelona waliweka rekodi ya kutwaa vikombe vyote sita ambavyo klabu hiyo ilishindania (Sextuple). Moja ya vikombe hivyo ni ligi ya mabingwa ulaya ambayo Barcelona ya Pique iliitoa Chelsea kwenye nusu fainali kwa faida ya bao la ugenini. Mchezo wa kwanza uliofanyika Nou Camp uliisha kwa sare tasa. Katika mchezo wa marudiano uliofanyika Stamford Bridge tarehe 6 May 2009, mwamuzi Tom Ovrebo  wa Norway alikataa penati nne za Chelsea ikiwemo moja ambayo yeye Pique aliushika mpira uliopigwa na Nikolas Anelka ambaye alikuwa akimpiga cheka Pique. Baada ya mchezo ule, Pique, alikiri kuushika mpira ule mbele kituo cha TV cha sky sports 2, “Kusema kweli mpira ule niliushika lakini sikudhamiria, mwamuzi anaweza akaamua anavyotaka na aliamua kuwa haikuwa penati  na inabidi kuheshimu maamuzi hayo. Wakati mwingine maamuzi huwa hayako sahihi  lakini  nina furaha kwa sababu tunakwenda fainali. Mambo mengine huwezi kuyadhibiti”  Mwisho wa msimu Pique na wenzake wakapongezana na kujisifu kwa kushinda ubingwa wa ulaya!



Gerard Pique akiunawa mpira ndani ya eneo la hatari huku mwamuzi  Tom Ovrebo akiangalia.








Msimu wake wa pili wa 2009-2010, katika mechi ya marudiano ya nusu fainali ya ligi ya mabingwa kati ya FC Barcelona na Inter Milan katika uwanja wa Nou Camp, tarehe 28 April 2010, mwamuzi wa kibelgiji Frank de Bleeckere alimpa kadi nyekundu Thiago Motta wa inter Milan kwa kilichoonekana kama kumpiga kiwiko Sergio Busquets wa Barcelona. Lakini kiukweli Motta hakumgusa Busquets, na hata kama angemgusa basi ingekuwa kifuani na sio usoni kama ambavyo Busquets alionesha. Mwisho wa mechi Barcelona walishinda 1-0 lakini haikutosha. Wakatolewa kwa jumla ya mabao 3-2.


Robin Van Persie akilalamikia maamuzi ya kupewa kadi nyekundu.









Msimu wa 2010-2011 katika mchezo wa marudiano wa hatua ya 16 bora ya ligi ya mabingwa baina ya FC Barcelona na Arsenal uliopigwa Nou Camp tarehe 8 March 2011, mwamuzi  Massimo Busacca kutoka Uswis alimpa kadi nyekundu Robin Van Persie wa Arsenal kwa kuupiga mpira wakati filimbi imekwishalia. Lakini kwa hali halisi, Van Persie asingeweza kujizuia kuupiga mpira ule. Kulia kwa filimbi na uamuzi wake wa kupiga mpira vilikwenda pamoja, hiyo ni mbali na kelele za mashabiki zaidi ya 95486 walioingia Nou Camp siku hiyo. Mpaka dakika hiyo, matokeo yalikuwa 1-1 na baada ya kadi nyekundu, Barcelona wakashinda 3-1 na Pique na wenzake wakajipongeza.  



Picha za marudio zikionesha hakukuwa na mgusano wowote kati ya Dan Alves na Pepe.










Msimu huo huo kwenye mchezo wya kwanza wa nusu fainali ya ligi ya mabingwa katika uwanja wa Santiago Bernabeu tarehe 27 April 2011 kati ya FC Barcelona na Real Madrid, mwamuzi Wolfgang Stark  kutoka Ujerumani alimpa kadi nyekundu kiungo wa Real Madrid, Pepe kwa kilichoonekana kumchezea madhambi Dani Alves wa FC Barcelona. Lakini marudio ya picha yalionesha Pepe hakumgusa Dani Alves. Kocha wa Real Madrid kwa hasira alimfuata mmoja wa waamuzi na kumpongeza kwa kumwambia “kazi nzuri” huku akimpigia makofi. UEFA walimmuadhimu Mourinho kwa kukiita kitendo kile ni dhararu kwa waamuzi. Mpaka kadi ile inatolewa matokeo yalikuwa 0-0, baada ya kadi hiyo Barcelona wakatumia nafasi na kushinda 2-0. Mwisho wa mchezo pique na wenzake wakapongezana.


 "Penati halali" ambayo iliwavusha FC Barcelona ya Gerard Pique kwenye robo fainali ya ligi ya mabingwa dhidi ya AC Milan.







Msimu wa 2011-12 katika mchezo wa marudiano wa robo fainali ya ligi ya mabingwa kati ya FC Barcelona na AC Milan kwenye uwanja wa Nou Camp tarehe 3 April 2012, mwamuzi Björn Kuipers  wa Uholanzi alifanya kioja cha mwaka. Dakika ya 40 wakati matokeo yakiwa 1-1, FC Barcelona walipata kona. Kabla kona haijapigwa, wakati wachezaji wanasukumana kutafuta nafasi, mwamuzi akatoa penati kwa Barcelona. Mwisho wa mechi Barcelona ikashinda 3-1. Pique na wenzake wakapongezana.

Hayo ni baadhi tu ya matukio ambayo FC Barcelona imefaidika nayo huku Pique akishuhudia. Ni matukio ambayo yaliwaathiri sana wapinzani na kuwaharibia malengo yao huku  Barcelona na Gerard Pique wakijipongeza na kujiita klabu bora kabisa duniani.

Kati ya watu ambao wamekutana na balaa mbele ya FC Barcelona ni Jose Mourinho ambaye kwa sasa ni kocha wa Real Madrid (japo ataondoka mwishoni mwa msimu) ambayo Pique alilalamika kwamba waamuzi wanaipendelea. Mourinho amekwisha kutana na kadi nyekundu 9  akiwa kocha wa timu tofauti kuanzia Chelsea, Inter Milan na Real Madrid. Kati ya hizo, 8 walipewa wachezaji wake na moja yeye mwenyewe (Simaanishi kwamba zote hazikuwa halali). Ndo maana tarehe 6 April 2010 mara tu baada ya kushinda mchezo wa marudiano wa robo fainali ya ligi ya mabingwa dhidi ya CSKA Moscow ya Urusi, Mourinho ambaye wakati huo alikuwa kocha wa Inter Milan, aliwaambia waandishi wa habari, “ tumejua kwamba tutacheza na Barcelona kwenye nusu fainali, kwa mara nyingine tena tutacheza tukiwa kumi (alimaansiha ni lazima kuna kadi nyekundu itatoka dhidi yao, na kweli ikatoka kwa Thiago Motta) kwa hiyo tunajiandaa kuikabili hali hiyo".


1 comment:

  1. I thіnk the admin of this websitе is really worκing hard in favоr оf his ωebsite, аs
    here еveгy stuff is quality based data.


    mу website ... hcg diet

    ReplyDelete