Juu Calvin Muro akiwa katika amelazwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili baada ya kujeruhiwa kwa risasi na askari wa kituo cha Polisi Mbezi kwa Yusuph jijini Dar es Salaam juzi.Picha na Abdallah Khamis
---
DAR ES SALAAM, Tanzania
MKAZI wa Mbezi kwa Yusuph Calvin Muro, amelazwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili baada ya kujeruhiwa na risasi zilizofyetuliwa na askari wa jeshi la Polisi kituo cha Mbezi waliokuwa katika harakati za kulikamata lori lililobeba Mchanga.
Akiwa kitandani katika hospitali hiyo ya Muhimbili, Muro alisema kuwa majira ya saa moja na nusu usiku aliwaona polisi wakiwa katika gari aina ya defenda wakilikimbiza lori la mchanga ambalo lilienda kupaki katika eneo la kimara B na dereva wake kukimbilia katika gesti ya Pentagon kwa ajili ya kujisalimisha.
Aliongeza kuwa askari waliokuwa wakimfukuza dereva huyo wa lori ambaye jina lake halikufahamika, walienda hadi katika gesti ya pentagon na kumkamata kisha wakaanza kumpiga kwa ngumi na teke
“Mwanzoni tulishangaa tukajua ni jambazi lakini tulipoona wanaanza kumpiga kwa mangumi na mateke ikatufanya na sisi tusogee kujua kinachoendelea ambapo tulimsikia yule dereva akilalamika kwa kusema sina pesa na ninatakiwa nipeleke hesabu ninyi mmezoea kutuonea”alisema Muro.
Alisema baada ya wananchi kusikia kauli hiyo walianza kuwazomea maaskari ambao waliondoka na baada ya muda wakarudi na kuanza kufyetua risasi hovyo na nyingine ndiyo ikampata chini ya makalio na kutokezea kwa mbele.
Sikuusikia mlio wa risasi bali nilijihisi kama ninavuja maji na nilipojisogeza katika mwanga nikaona tundu kubwa limejitokeza mbele ya paja langu huku damu ikinivuja kwa wingi ndipo wenzangu waliponichukua na kunipeleka Polisi kisha hospitali ya tumbi kibaha ambao nao walinihamishia hapa Muhimbili majira ya saa nane usiku”aliongeza kusema Muro kwa taabu.
Aliongeza kuwa baada ya kutembea kama hatua kumi huku wakiwa wamewasha indiketa ya gari lao kuashiria wanaelekea kituo cha polisi Mbezi kwa Yusuph Mmoja wao alielekeza bunduki upande wa gesti ya Pentagon na kisha kufyetua bomu la machozi kabla ya wenzao kuanza kurusha risasi iliyompata Calvin Muro.
“Hawa wamezoea kukamata malori na kuchukua rushwa na huwa wana vizuizi vyao tunawajua sasa katika hili yule dereva alikataa kusimama nao kwa hasira wakaamua kumfuata na kumshushia kipigo”alieleza shuhuda huyo.
Mkuu wa Polisi wilaya ya Kimara aliyefahamika kwa jina moja la Papalika,alipoulizwa kuhusiana na tuhuma za askari wake kutumia risasi kwa ajili ya kulazimisha rushwa alikataa kutolea maelezo na kutaka atafutwe kamanda wa Polisi mkoa wa Kinondoni.
“Msemaji ni afande Kenyela mimi taratibu haziniruhusu kutolea maelezo hayo unayoniuliza lakini kama askari wetu wanahusishwa na rushwa tutafanyia kazi na ukweli utajulikana”alisema SP Paparika.
Jitihada za kumpata kamanda wa Polisi mkoa wa Kinondoni zilishindikana baada ya namba zake ambazo ni O754 485911 na 0784 820033 kutopatikana hewani huku baadhi ya maaskari wakiahidi kumueleza kupitia simu zao za redio kuwa anatafutwa na waandishi wa habari. Askari hao walikuwa katika gari lenye namba za usajili Polisi PT 1412.
No comments:
Post a Comment