Wednesday, January 11, 2012

MIAKA 50 UHURU; UGALI NI ULE ULE:

Ndugu zangu,

Nimetafakari sana  na kujiuliza; kwanini  hata katika miaka 50 ya uhuru  wetu hatujaweza kubadilisha hata ladha ya ugali tunaokula?

Ndio, miaka 50 ya Uhuru na ugali ni ule ule.  Hatujaongeza ubora wa ugali wala wingi wake kwenye sahani. Kama jana kama leo, tunachemsha maji, tunaweka unga  na kisha tunasonga.  Ni vile vile, tunasonga ugali kwa mazoea. Hivi, hatuwezi  kuukamulia ndimu au limau ugali tunaousonga?

Ni swali linalokutaka ufikiri kwa bidii. Maana, kama tunaweza kunywa uji wa ndimu au limau kwanini tusiweze kula ugali wa ndimu au limau? Naam, ndimu inaweza kuchangamsha ugali tunaokula.

Na kama tunaweza kunywa uji wa chenga kwanini tusianze kusonga ugali wa chenga? Na ugali wa chenga ukikamuliwa ndimu au limau unaweza kuwa mtamu haswa.

Ndugu zangu,
Tunahitaji mabadiliko.
Tumekuwa ni watu wa kuogopa mabadiliko. Ni watu tulioridhika na ugali ule ule, miaka nenda miaka rudi. Kwanini? Tumekuwa kama watu wa Taifa la Kusadikika. Maana, mwandishi yule mahiri, Mtanzania mwenzetu Shaaban Robert anaandika; ” Wasadikika wana desturi ya kutafuta fimbo baada ya kuumwa na nyoka. Tumekwisha umwa na nyoka wa  matendo yetu mabaya ya zamani.
 
Nyoka mwenyewe amekwishakimbia. Hapatikani kwa kujilipiza kisasi, lakini, sumu yake imebakia katika jeraha  tulilolipata. Sasa, shauri lililo jema  ni kuzuia sumu hii isienee miilini mwetu ikaleta kifo.
Maovu yana hatari kubwa kukaa kati yetu. Tumedumu nayo kwa muda mrefu. Hayakutuletea faida ila hasara, huzuni na kilio siku zote.”- Shaaban Bin Robert.

Naam, na Shaaaban Robert naye alitutaka tubadilike, miaka 50 iliyopita!

Maggid Mjengwa,
Iringa
Januari 9, 2012 

No comments:

Post a Comment