Tuesday, December 13, 2011

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA MBUNGE WA KYELA, DK HARRISON MWAKYEMBE, AREJEA NCHINI:

NAIBU Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe.
 Naibu waziri wa ujenzi, Dr.Harrison Mwakyembe, akielekea kula kiapo siku chache baada ya kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete Mwaka Jana.
---

NAIBU Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe, amerejea nchini akitokea Hospitali ya Apollo nchini India alikolazwa kwa ajili ya matibabu ya ugonjwa wa ngozi. Dk Mwakymbe aliondoka nchini Oktoba 9 mwaka huu kwenda nchini India baada ya hali yake ya afya kuzorota huku ngozi yake ikionekana kudhoofika.

Baada ya kukaa India kwa takriban miezi miwili, jana saa 7:00 mchana, Dk Mwakyembe aliwasili nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere kwa ndege ya Shirika la Qatar Airways.

Habari zilizolifikia jana mchana zilieleza kuwa baada ya kutua jijini Dar es Salaam, Dk Mwakyembe aliondoka moja kwa moja kuelekea mkoani Mbeya. Akizungumza jijini Dar es Salaam jana,Msemaji wa Familia na Mbunge wa Lupa,Victor Mwambalaswa alisema, afya ya mbunge huyo wa Kyela, ni nzuri ndio maana ameruhusiwa kutoka hospitali.

“Ni kweli Dk Mwakyembe amerejea nchini salama.Tunamshukuru Mungu, hii inatokana na madaktari waliokuwa wakimpatia matibabu kumpa ruhusa baada ya kuona hali yake ni nzuri na kwamba anaweza kuendelea na majukumu yake kama kawaida,” alifafanua Mwambalaswa na kuongeza:

“Kutokana na hali hiyo, tunaamini kuwa, kurudi kwake nchini, kutaleta matumaini mapya ya afya yake.” Msemaji huyo wa familia alisema, baada ya kurudi, Dk Mwakyembe atapumzika kijijini kwao Kyela ili aweze kujumuika na wanafamilia katika kipindi hiki cha Sikukuu ya Chrismasi na mwaka mpya, kabla ya kuanza kazi rasmi ya ujenzi wa taifa mwakani.

No comments:

Post a Comment