MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad akivishwa nguo ya kuokolea maisha (life jacket) na askari wa kikosi cha kuzuia Magendo (KMKM), alipokuwa akitaka kupanda boti kuelekea kisiwa kidogo cha Kojani, mkoa wa Kaskazini Pemba jana. Picha na Salmin Said, Ofisi Ya Makamu Wa Kwanza Wa Rais
----
*Ataka zitumike kuinua maendeleo ya jamii
*Asema siri ya maendeleo amani, utulivu uliopo
*Asema siri ya maendeleo amani, utulivu uliopo
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema wakulima wa karafuu kisiwani Pemba wanatarajiwa kutia mifukoni kiasi cha shilingii bilioni 50 hadi mwishoni mwa msimu wa zao hilo mapema mwakani, na kuwahimiza fedha hizo zitumike kwa maendeleo na wajiepushe na tabia ya kuzitumia kwa kuongeza wake bila sababu za msingi.
Maalim Seif alisema mafanikio hayo kwa wakulima wa karafuu wa Zanzibar ni matokeo ya utekelezaji ahadi za serikali za kuhakikisha wananchi wanakuwa na maisha bora, wakiwemo wakulima, wafanyakazi na wavuvi, ambao ndio wanaochukua asilimia kubwa ya wananchi wa Unguja na Pemba.
Alisema serikali ya awamu ya saba iliazimia kupandisha bei ya mazao mbali mbali, ikiwemo la karafuu kwa nia ya kumuona mkulima ananufaika na mazao yake kwa asilimia 80, ambapo hivi sasa wakulima wa karafuu wanauza karafuu zao kilo moja daraja la kwanza kwa shilingi 15,000 kutoka shilingi 5000 msimu uliopita.
Alisema hayo jana alipowahutubia wananchi wa kisiwa kidogo cha Kojani, mkoa wa Kaskazini Pemba akiwa katika ziara ya siku nne kisiwani Pemba.
Makamu wa Kwanza wa Rais alisema bei nzuri ya karafuu ni neema kubwa kwa wakulima kwa sababu huko nyuma wakulima walikuwa hawapati hata asilimia 30 ya mapato yatokanayo na mazao yao, lakini hivi sasa baada ya serikali kuona umuhimu wa mkulima kunufaika na imeweza kupandisha bei katika kiwango kwenye maslahi.
“Mkulima wa karafuu sasa anapata asilimia 80 ya mazao yake, tunatarajia hadi mwishoni mwa msimu huu wa karafuu bilioni 50 zitakuwa zimeingia Pemba, zitumie fedha hizo kwa mambo ya maendeleo, na sio kuoa wake wengi zaidi bila ya sababu za msingi”, alisema Maalim Seif.
Alisema baada ya mafanikio kuanza kupatikana katika zao la karafuu, serikali inaelekeza nguvu kubwa katika zao la mwani, ambalo hadi sasa wanunuzi wanawalipa wakulima kwa bei ya chini, ambayo hailingani na kazi wanayoifanya pamoja na kulihudumia hadi kufikia hatua ya kuwauzia wafanyabiashara hao.
Akipokuwa katika ziara katika kisiwa kidogo cha Tumbatu, wiki mbili zilizopita, Makamu wa Kwanza wa Rais alisema serikali itaendeleza mazungumzo na wanunuzi wa zao la mwani kuwataka wapandishe bei angalau ifike shilingi 1000, lakini iwapo watakataa, serikali itafikiria zao la mwani linunuliwe na serikali kupitia Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC), kama inavyofanya kwa zao la karafuu.
Akielezea mafanikio mengine ya serikali hii ya awamu ya saba yenye mfumo wa umoja wa kitaifa alisema ni kuongeza mishahara ya watumishi wa umma kwa asilimia 25, kiwango ambacho ni kikubwa na kwamba ni nchi chache zinazoweza kuongeza mshahara katika kiwango kama hicho kwa mara moja.
Maalim Seif alisema nyongeza hiyo ya mshahara inakwenda sambamba na kulipwa wafanyakazi ambao kwa muda mrefu walikuwa hawajapewa nyongeza zao, ambapo pia mafao ya kada muhimu kama vile madaktari yameongezwa, ili kwenda sambamba na majukumu mazito wanayoyakabili, lakini pia walingane na wenzao wa Tanzania Bara.
Alisema baada ya hatua hiyo ya kuzingatiwa mafao ya madaktari hakuna sababu hivi sasa wakahamie sehemu nyengine kama vile Tanzania Bara kwa sababu maslahi ambayo wangeweza kuyapata huko wanalipwa hapa hapa Zanzibar.
Akizungumzia sekta ya uvuvi, Maalim Seif alisema matumaini makubwa ya mafanikio yameanza kujengeka kufuatia juhudi zinazoendelea kuchukuliwa kuvutia wawekezaji katika sekta hiyo, ambao wataweza kuwanufaisha wavuvu wadogo wadogo wa Unguja na Pemba.
Aliwaleza wananchi wa Kojani ambao asilimia kubwa ni wavuvi kuwa, baadhi ya wawekezaji wa sekta hiyo tayari wameonesha nia ya kuja kufungua viwanda vya kusindika samaki, kutengeneza boti za kisasa kwa ajili ya wavuvi wadogo wadogo wa Zanzibar pamoja na kuleta meli kwa ajili ya shughuli za uvuvi wa bahari kuu, ambapo wavuvi wa Zanzibar ndio walengwa wakuu wa ajira katika meli hizo.
Huku akishangiriwa na wananchi waliojitokeza kwa wingi katika mkutano huo wa hadhara, Maalim Seif alisema mbali na wawekezaji katika sekta ya uvuvi kuonesha dhamira za kuja kufungua miradi Zanzibar, juhudi nyengine zilizokwisha chukuliwa na serikali ni kuwapeleka wavuvi kutoka vikundi mbali mbali vya Zanzibar nchini China kujifunza mbinu za kufuga samaki na baadaye wao wawafundishe wananchi wengine.
Hata hivyo, alionya kwamba juhudi hizo zitakuwa na mafanikio makubwa iwapo wananchi wa Zanzibar watatoa kipaumbele katika kuyalinda na kuyahifadhi mazingira ya bahari kwa kujiepusha na aina zote za uvuvi haramu na uharibifu wa matumbawe ambayo ndiyo mazalia ya samaki na kuepuka kukata miti ya mikoko.
Maalim Seif alisema kwamba siri kubwa ya mafanikio yaliyoanza kujitokeza Zanzibar ni kuendelea kudumisha amani na utulivu tokea kufikiwa maridhiano ya kisasa na kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa ambayo hivi sasa imetimiza mwaka mmoja na kuhimiza wananchi wote kuhakikisha umoja na mshikamano huo unalindwa, ili kuleta mafanikio zaidi.
Na
Na Khamis Haji,
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais,
Pemba.
No comments:
Post a Comment