Mbunge wa Ubungo-Chadema,Mheshimiwa John Mnyika.
---
Kurugenzi ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa ya CHADEMA inaitaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa tamko juu ya kauli ya Waziri wa Ulinzi wa Israel ya kwamba nchi yetu si ya muhimu wala ya maana.
Waziri Barak alifanya mahojiano na Radio Israel na kutoa kauli ambayo imenukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari vya nchi hiyo wiki iliyopita kuwa “ Germany, France and England are not Tanzania, Mauritania or Tripolitania…..these are very important, very relevant countries and we don’t have an interest in increasing tensions with them or making them bitter enemies”.
Kwa kauli hii serikali ya Israel inaiona Tanzania sio nchi ya muhimu wala ya maana hata kufikia hatua ya kuilinganisha na eneo tu ndani ya Libya linaloitwa Tripolitania.
Tunamtaka Waziri wa Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa, Benard Membe kuitaka serikali ya Israel kuomba radhi kufuatia kauli hiyo au kueleza wazi iwapo mazungumzo hayo ya Waziri Barak ni msimamo wa nchi hiyo kuhusu uhusiano wa kidiplomasia wa mataifa yetu.
Barua pekee ya balozi wa heshima wa Tanzania nchini Israel, Kasbian Nuriel Chirich kwenda kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Avigdor Lieberman ya kulaani matamshi hayo ya Waziri Barak na kumkaribisha mwakilishi wa Israel kutembelea Tanzania haitoshi kuifanya serikali ya nchi hiyo kutambua athari za kidiplomasia za kauli iliyotolewa.
Aidha kwa kuwa serikali imekuwa ikieleza kwamba Tanzania ina mahusiano mazuri ya kiulinzi na Israel, ni muhimu pia Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dr Hussein Mwinyi akaeleza umma iwapo kauli hiyo ya Waziri Barak ndio msingi wa mahusiano yaliyopo kati ya nchi zetu kuhusu ulinzi na usalama.
Kurugenzi ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa inachukua fursa hii kurudia kuwakumbusha watanzania kwamba kupuuzwa huku kwa nchi yetu katika medani ya kimataifa kunatokana na sera mbovu ya mambo ya nje chini ya utawala wa sasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Tanzania imepoteza heshima katika siasa za dunia kutokana na diplomasia yetu kujikita katika kuomba omba kimataifa; pamoja na kuwa kimaneno na maandishi serikali inazungumza kuhusu diplomasia ya kiuchumi, kivitendo mahusiano yetu yamejengeka katika misingi ya utegemezi, kupungua kwa urari wa kibiashara na kuachia mianya ya uporwaji wa rasilimali.
Kurugenzi ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa inatambua kwamba wakati wa uongozi wa awamu ya kwanza wa hayati Mwalimu Julius Nyerere, Tanzania ilikuwa na heshima na sauti kimataifa sio tu katika jitihada za ukombozi kusini mwa Afrika bali pia katika mahusiano ya kisiasa, kiuchumi na kijamii baina ya nchi za kusini na mataifa mengine duniani.
Hali ya Tanzania kupoteza sauti katika medani ya kimataifa imedhihirika pia hivi karibuni katika mkutano kuhusu mabadiliko ya tabia nchi (COP 17) uliomalizika hivi karibuni nchini Afrika Kusini; wakati nchi yetu ikiwa ni miongoni mwa waathirika wakubwa zaidi wa mabadiliko ya tabia nchi. Iwapo hatua hazitachukuliwa kurejesha heshima na sauti ya Tanzania kimataifa maamuzi mengi yatafanyika yenye athari kwa wananchi wengi bila ushiriki wao thabiti kama yanayoendelea hivi sasa kuhusu Mikataba ya Kiuchumi na Nchi za Jumuia ya Ulaya (EPA) yenye madhara kwa wakulima na wenye viwanda nchini.
Kurugenzi ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa inatoa mwito kwa watanzania kuendelea kuunganisha nguvu ya umma kusimamia uwajibikaji na kufanya mabadiliko ya kimsingi ya kiuongozi, kisera na kimfumo ya kitaifa ili kuweza kurejesha nafasi na heshima ya Tanzania kimataifa katika mazingira ya sasa ya ushindani wa kiuchumi, kiulinzi, kijamii na kisiasa.
Kauli ya Waziri Barak nimuendelezo tu wa mataifa mbalimbali kuifanya Tanzania na baadhi ya nchi nyingine za Afrika kuwa hazina heshima wala sauti katika siasa za kimataifa kama ambavyo Serikali za Uingereza na Marekani zimeweka masharti yenye mwelekeo wa ukoloni mamboleo kuhusu masuala ya ushoga na usagaji.
Hatua za kupinga kauli za kudharauliwa na kulazimishwa mambo tusiyoyataka ziende sambamba na kudhibiti mianya yote ya ufisadi wa kimataifa, uwekezaji uchwara na kutetereka kwa misingi wa utawala wa kisheria masuala ambayo yanasababisha migogoro na pia rasilimali za nchi kutokutumika kwa manufaa ya wananchi walio wengi; tukijiheshimu, tutaheshimiwa.
Wenu katika Demokrasia na Maendeleo,
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa (CHADEMA)
No comments:
Post a Comment